Site icon A24TV News

HUKUMU YA SABAYA YAGONGA MWAMBA MPAKA JUNI 10 2022

Na Mwandisho wa A24Tv
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akishuka kwenye gari la Magereza akiingia Mahakamani
Arusha.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeahirisha hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita kutokana na Hakimu kuwa na majukumu mengine.
 Akiahirisha kesi hiyo leo Jumanne Mei 31, 2022, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Fadhil Mbelwa amesema shauri lilipangwa kwa ajili ya hukumu ila hakimu aliyekuwa akiisikiliza amepangiwa majukumu mengine ya kikazi nje ya ofisi.

“Shauri linakuja kwa ajili ya hukumu na liko kwa Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda lakini siku ya leo amepangiwa majukumu mengine ya kikazi nje ya ofisi hataweza kutoa hukumu leo hadi Juni 10, 2022,” amesema Hakimu huyo

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021, mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Leo Jamhuri iliwakilishwa na Mawakili wa Serikali waandamizi Janeth Sekule, Felix Kwetukia, Wakili wa Serikali Neema Mbwana na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Jacopiyo Richard.

Utetezi uliwakilishwa na Mawakili Mosses Mahuna, Fridolin Bwemelo, Edmund Ngemela na Sylvester Kahunduka ambao wanawatetea washitakiwa sita isipokuwa Mwahomange ambaye anajitetea mwenyewe mahakamani hapo