Na Mwandishinwa A24Tv Arusha
Aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima (44) na wenzake wawili leo Juni 22, 2022 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi yenye mashtaka sita ikiwemo mawili ya utakatishaji fedha.
Wengine ni Mariam Mshana (40), aliyekuwa mkuu wa idara ya fedha ya halmashauri hiyo na Innocent Maduhu (40) aliyekuwa mkuu wa idara ya mipango ya uchumi.
Mbali na watuhumiwa hao, wengine ni Nuru Ginana na Alex Daniel ambao walikuwa wachumi katika jiji hilo, nao walifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kukamilisha dhamana ambapo kupitia mawakili wao waliieleza mahakama hiyo kuwa hawajakamilisha masharti ya dhamana.
- Katika a kesi hiyo Jamhuri inawakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule, Wakili wa Serikali, Charles Kagilwa na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Richard Jacopiyo huku washtakiwa hao wakiwakilishwa na Mawakili Valentino Nyalu na Sabato Ngogo.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022, washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita ambapo kosa la kwanza linalowakabili ni ufujaji na ubadhirifu wa Sh103 milioni, kosa la pili na la tatu ni kutumia nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri.
Kosa la tano linalomkabili Maduhu ni utakatishaji fedha huku la sita likiwa utakatishaji ambalo linawakabili wote watatu.
Wote walikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa Jamhuri ulieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na hakimu
Mwakisu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 5, 2022.