Site icon A24TV News

HALMASHAURI YA ARUSHA KITANZINI, YAAMURIWA KULIPA BIL.1.7 BAADA YA KUVUNJA NYUMBA ZA WANANCHI

Na Joseph Ngilisho,Arusha
Kaya zaidi ya 280 zimeathirika  Kisaikolojia baada ya nyumba zao za kuishi na biashara walizojenga katika barabara Mianzini- Timbolo  kuvunjwa na Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru Mkoani Arusha na kufanya kuishi kwa kubangaiza .
Waathirika hao wamemwomba  Rais Samia Suluhu Hassan aweze kuwasaidia kulipwa fidia ya shilingi bilioni 1.7 baada ya kushinda kesi mahakamani na halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia .
Nyumba 43 zilibomolewa na wananchi hao wamekuwa wakihangaika kule ya huko kutafuta haki lakini viongozi wa Halmashauri ya Arusha imekuwa ikiziba masikio na kuwaacha kama yatima na wasijue la kufanya.
Ombi hilo,wamelitoa kwa Rais Samia baada ya wananchi hao kushinda kesi katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa lakini halmashauri hiyo, imeshindwa kutekeleza agizo la mahakama .
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika eneo la tukio la uvunjwaji nyumba Mwenyekiti wa wananchi hao,Fanuel Titus Lamai ambaye ni Mwenyekiti wa Wahanga alisema walivunjiwa nyumba kutokana na kupanuliwa kwa barabara lakini Mahakama ilisema katika hukumu zake kuwa barabara ilifuata watu hivyo wananchi hao wanapaswa kulipwa fidia na sio vinginevyo.
Lamai alisema Jaji wa Mahakama Kuu Jaji Fatuma Masengi na Majaji watatu katika Mahakama ya Rufaa walieleza wazi katika maamuzi ya hukumu zao kuwa wananchi hao wanapaswa kulipwa fidia kwa kuwa nyumba zilikuwa nje ya sheria ya barabara hivyo barabara iliwafuta watu na wanapaswa kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
“Tunaiomba serikali yetu sikivu chini ya Rais Samia itusaidie tupate haki yetu kwa kuwa tangu mwanzo tulishinda mahakamani ila kumekuwa na shida kwenye utekelezaji wa amri ya mahakama.
“Tunaomba atusaidie tulipwe pesa zetu kwa ni haki yetu kwani baadhi yetu wamekufa kwa mshituko na wengine wamepooza mwili na hawajui la kufanya na wengine walikopa benki kujenga nyumba za kuishi na biashara sasa wako taababi kimaisha hawajui la kufanya’’alisema Lamai
Akizungumzia sakata hilo, alisema ilikuwa mwaka 2011 walipewa taarifa na halmashauri ya Arusha, kuvunja nyumba zao kando kando ya barabara kwa kuwa barabara ilitakiwa kupanuliwa.
Alisema walipopewa  taarifa hizo, waliona hawajetendewa haki kwa kuwa wako nje ya barabara na wako nje ya barabara kwa mujibu wa sheria na walikwenda Mahakamani kufungua kesi na Mei 26 mwaka 2014 mbele ya Jaji Msengi walishinda na ilitakiwa walipwe fidia.
Alisema baada ya Jaji kutoa hukumu hiyo na wananchi hao kupeleka madai ya shilingi bilioni 6.8 ya wananchi 38 lakini Mthamini Mkuu wa Serikali alifanya Tathimini ya wananchi 32 waliokithi vigezo na kuitaka Serikali kuwalipa wananchi shilingi bilioni 1.7 tu na sio vinginevyo kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti huyo alisema baada ya hukumu halmashauri ya Arusha walikwenda Mahakamani na kudai kuwa hawakuwa na fedha za kufidia na Julai 7 mwaka 2015 mahakama ilitoa uamuzi kuwa kama hawana fedha basi barabara ibaki kama ilivyokuwa mwanzo kwa upana wa mita nane hadi hapo watakapolipa fedha za fidia.
Alisema mwaka 2016 Halmashauri ya Arusha ilikaidi amri ya Mahakama na kuamua kuwavamia na kuvunja nyumba zote zilizokuwa katika barabara Mianzini –Timbolo bila ya kuwafidia na wananchi hao walirudi tena Mahakamani na kesi ilisikilizwa Mahakama ya Rufaa Arusha chini ya majaji wa tatu na Agosti 25 mwaka 2020 walitoa uamuzi kuwa wananchi hao wanastahili kulipwa fidia
Naye Susan Joseph, mhanga wa sakata hilo mkazi wa Ilboru Wilayani Arumeru,alisema wamepata matatizo makubwa kutokana na uamuzi wa Halmashauri ya Arusha kuvunja nyumba zao bila kulipwa fidia kwani wengine walijenga nyumba za biashara na wengine walijenga nyumba za kuishi.
“Nikweli tumeathiri kutokana na adha hii, kwa kuwa mimi na familia yangu wakiwamo wajukuu ambao nawalea tulikuwa tunategemea kujikimu kimaisha,pia nilikuwa na mikopo mingi benki na baada ya kuvujwa nilishindwa kurejesha mkopo ya fedha niliyochukua na maisha yamekuwa magumu hivyo tunaomba Rais asikilize kilio chetu,”alisema.
Naye Agness Mollel,alisema hali ya utengenezaji wa barabara hiyo,imemuathiri sana kwa kuwa alikuwa mtumishi serikalini katika Halmashauri ya Jiji la Arusha na alipopewa fedha za kustaafu  alizitumia kujengea vyumba vya biashara vinne kando ya barabara hiyo.
Alisema kubomolewa kwa nyuumba yenye vyumba hivyo kumefanya kubaki katika hali ya ukiwa,shida na njaa kwa kuwa hana kitu cha kula alikuwa anategemea vyumba hivyo.
Akizungumzia sakata hilo Mwanasheria wa Halmashauri ya Arusha,Monica Mwailolo alisema kuwa kesi hiyo walikuwa wakishirikiana na ofisi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwa maamuzi mapya ya Jaji Judith Kamala yaliyosistiza wanachini hao lazima walipwe fidia lazima awasiliane na ofisi hiyo kwa maamuzi zaidi.
Mwailolo alisema kwa sasa sina la kujibu zaidi ya kusema kuwa atakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo pale watakapo kaa na kutoka na maamuzi ya pamoja.
Ends…