Na JosephNgilisho,Arumeru
Kamati ya kudumu ya bunge ya katiba na sheria imewashauri wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu hapa nchini kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuwekeza akiba ya fedha kwa ajili ya matumizi ya baadaye ikiwemo mitaji ya kujiajiri pindi wanapohitimu masomo yao
Akiongea na wanafunzi wa chuo kikuu cha Arusha (UOA)baada ya kutembelea chuoni hapo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kujiunga na mfuko wa hifadhi wa NSSF,mbunge wa viti maalumu mkoani Mbeya(CCM),Suma Fyandomo aliwataka vijana waliopo kwenye vyuo vikuu nchini kutumia sehemu ya fedha wanazopata kutoka bodi ya mikopo nchini(Heslb) kujiwekea akiba na sio kuzifanyia starehe.
Fyandomo,alisema kwamba kumekuwa na tatizo kubwa la ajira kwa vijana nchini na kuwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kujiwekea akiba ili baadae waweze kupata mitaji ya kujiajiri kwa maisha ya baadae na kuachana na dhana ya kusubiri ajira kutoka serikalini.
“Vijana wajitokeze kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kwa malengo ya baadae hata wale wanaopokea fedha kutoka bodi ya mikopo wanaweza kuweka akiba kidogokidogo na wakihitimu wanaweza kupata mitaji kupitia akiba waliyojiwekea”alisema Fyandomo
Naye Mbunge wa jimbo la Mwanga,Joseph Tadayo alisema kwamba ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anajijengea utamaduni wa kujiweka akiba huku akizitaka taasisi za kiraia kuhamasisha utamaduni huo tangu wakiwa shule za msingi na sekondari.
Mkuu wa chuo kikuu cha Arusha,Prof Patrick Mano aliwataka wanafunzi wa chuo hicho kuanza kujenga desturi ya kujiwekea akiba na kusisitiza kuwa ni aibu kwa mwanafunzi wa ngazi ya chuo kikuu kutokuwa na akiba yoyote ya benki.
Aidha aliwashauri wanafunzi hao kuwa na utamaduni wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kujiwekea akiba ya baadaye na kuacha kutumia ovyo fedha za mkopo na zile wanazopewa na wazazi wao kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Makamu mkuu wa chuo kikuu cha Arusha,Prof Kitojo Wetengele alisema kwamba mpango wa kuwahamasisha wanafunzi wa chuo hicho kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini utakwenda kuwanufaisha kwa kuwaandaa kwa maisha ya baadae.
Ends….