Site icon A24TV News

Mbunge alia na barabara ya mchepuko kukwepa maporomoko ya Sonni

Na Joseph Ngilisho, Lushoto.

Mbunge wa Jimbo la Lushoto,mkoani Tanga,Shaaban Shekilindi ameishauri serikali kukamilisha ujenzi wa barabara ya mchepuko kwa kiwango cha Lami ili kuondoa changamoto ya Mara kwa Mara inayotokana na maporomoko ya mawe kwa barabara kuu inayotoka Mombo Hadi Lushoto ambayo imekuwa kilio kikubwa kwa wafanyabiashara wa mazao na mbogamboga pindi inapoziba.

Aidha ameishauri serikali kuangalia namna ya kuwachukukia hatua Kali makandarasi wanaochelewesha miradi mbalimbali ya maendeleo na kusababisha wananchi kuendelea kuteseka kwa kukosa huduma ya usafiri Katika wilaya hiyo.

Shekilindi ametoa kilio hicho mwishoni mwa wiki mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa,Sahili Geraruma wakati Mwenge wa Uhuru ulipofika jimboni kwake kutembelea,kuzindua na kuweka jiwe la msingi Katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa akilalamikia serikali na Bungeni mradi wa barabara ya mchepuko yenye urefu wa kilometa 16 inayoanzia Dochi kupitia  Nguli hadi Mombo ili kuwarahisishia wananchi na wafanyabiashara wanaosafirisha mazao kupita kwa urahisi tofauti na ilivyo sasa.
Alisema kuwa wananchi wa maeneo hayo wanategemea barabara moja pekee inayotoka Mombo kupitia Sonni hadi Lushoto barabara ambayo kunapotokea maporomoko barabara hiyo huziba na kutopitika na hivyo kuwa changamoto kubwa kwa wananchi na Wafanyabiashara.
Akiongelea suala la wakandarasi wanaotekeleza miradi  Katika Jimbo lake ,alisema wamekuwa changamoto ya ucheleweshaji wa miradi ya barabara kutokana na visingizio kadhaa visivyo na tija hivyo amewataka wakandarasi hao kumaliza kazi kwa wakati Kama mkataba unavyoeleza na kusema changamoto zilizo Nje ya Mkataba hazitakubalika kwani ni kuwaweka wananchi Katika hali mbaya kiusafiri.
Naye mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya  KIV  (KIV Company LTD) , Joseph Malumbo ,anayetekeleza mradi wa barabara yenye urefu wa kilometa moja  kwa kiwango Cha lami,alimshukuru kiongozi wa mbio za mwenge ,kuutembelea mradi huo na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Malumbo aliongeza kuwa mradi huo unagharimu kiasi Cha Shilingi milioni 493,271,000 alitarajia kukamilisha juni 19 Mwaka huu lakini kutokana na changamoto ya mvua  na kuhamisha udongo unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Naye kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Sahili Geraruma aliwataka wakandarasi hao kuhakikisha wanakamilisha miradi ya serikali kwa wakati na kwa kuzingatia ubora unaohitajika na wawe wazalendo kwa sababu wao ni  wazawa.
Mkuu wa wilaya ya Lushoto,Kalisti Lazaro alisema kuwa atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kiongozi wa mbio za mwenge 2022, ikiwemo matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na serikali na ubora wa mradi.