Na Geofrey Stephen .Arusha
Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatii katika maeneo mbalimbali nchini,Serikali imezindua miongozo kitaifa wa uundaji na uendeshaji wa mabaraza ya watoto Tanzania pamoja na madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto ndani na nje ya shule.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa sita wa wadau wa elimu kutoka nchi tatu za jumuiya ya afrika Mashariki,Kamishna wa ustawi wa jamii wa wizara ya maendeleo ya jamii,jinsia wanawake na makundi maalum,DK Nandera Muhando amesema miongozo hiyo ni moja ya mikakati ya kusaidia kupunguza ukatili kwa watoto.
“Miongozo hii ni muhimu katika kuweza kutusaidia kuwafikia hao watoto lakini pia na wanawake kwani sisi tumepewa jukumu kubwa la kumlinda mtoto chini ya sheria namba 21 ya 2009 pamoja na marekebisho madogo ya mwaka huo ambapo tutamlinda katika makao mbalimbali,nyumba salama na walioko mitaani,”amesema Dk.Muhando.
“Tumeamua kubadilisha uzoefu ili shule ziwe salama kwa watoto kujifunza pamoja na kuwaondolea hofu pindi wanapoenda na kurudi shuleni kwani pamoja na uwepo wa sheria mbalimbali bado vitendo hivyo vimekithiri katika baadhi ya maeneo mbalimbali,”amesema Dk.Kalage.
Aidha amesema kupitia kukithiri kwa matukio ya ukatili kwa watoto na wanawake imepelekea kutafuta mbinu shirikishi kutoka katika nchi zilizoendelea ili kuweza kujifunza namna ya kuzuia kwa lengo la kupunguza vitendo hivyo katika jamii.
Dk.Kalage amewataka wananchi kuendelea kufichua na kutaoa taarifa katika vyombo husika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake dhidi ya mtuhumiwa na vitendo vya ukatili viweze kupungua na watoto waweze kuwa salama na kujifunza ipasavyo.
Naye Afisa ustawi wa jamii wa mkoa wa Arusha,Dinis Mgiye amesema anashukuru wadau kwa kushirikiana na serikali kuzindua miongozo hiyo iliyolenga katika kuhakikisha watoto wanalindwa lakini bado wanaendelea kupambana na masuala ya ukatili.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau wanafanya juhudi katika kukabiliana na vitendo hivyo lakini changamoto ni baadhi ya familia kumalizia kesi nyumbani hali ambayo inachangia kuongezeka kwa matukio hayo,”amesema.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo,Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii kutoka halmashauri ya Arusha,Angela Mvaa amesema wamekuwa wakikabiliana na vitendo vya ukatili kwa kushirikiana na jamii.
Mwisho