Site icon A24TV News

THIBITINI UBORA BADALA YA KUDHIBITI BUNIFU – PROF MDOE

Na WyEST,

DODOMA.

Taasisi na Mamlaka za Uthibiti ubora wa bidhaa na huduma zimeshauriwa kuangalia upya sheria wanazozitumia ili kuhamasisha ubunifu na kulinda wabunifu wachanga.

Ushauri huo umetolewa Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe wakati akifungua kikaokazi cha kupitia Mwongozo wa Kitaifa wa Kuibua, Kutambua na Kuendeleza Ugunduzi, Ubunifu na Maarifa Asilia wa Mwaka 2018.

Prof. Mdoe amesema kazi za taasisi hizo ni kuthibiti ubora kwa maana ya kuhakikisha huduma na bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kusaidia wabunifu wachanga kufikia ubora na viwango vinavyotakiwa ili bunifu zinazobuniwa ziweze kumsaidia mbunifu mwenyewe, jamii na Taifa.

“Ujumbe wangu ninaoupeleka kwa Regulators tena leo nafahamu kwa asili ya sheria zilizounda taasisi hizi za Uthibiti ubora zimekaa kipolisipolisi na hazihamasishi ubunifu kwa hiyo kama mtu akija na kitu chake amekibuni yaani kitu cha kwanza anaulizwa una leseni? Umelipia?” amefafanua Prof. Mdoe.

Prof. Mdoe amesema wabunifu wachanga wanatakiwa kupewa miongozo ya namna bora ya kuboresha bunifu zao ili kufikia viwango vya ubora vya bidhaa na huduma hivyo taasisi husika zina wajibu wa kuondoa changamoto zinazowakabili.

“Wabunifu hawa ili waweze kufika malengo yao wanahitajika kushikwa mkono, changamoto zinaweza kumkatisha tamaa na kuamua kuacha kuendelea na shughuli za kiubunifu,” amebainisha Prof. Mdoe.

Aidha, amesema Mwongozo huo unaopitiwa una lengo la kumwezesha mbunifu kuanza kunufaika mwenyewe, jamii na taifa, ambapo mpaka sasa umewezesha kuibuliwa kwa wabunifu wapatao 2,647 kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU).

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Prof. Maulilo Kipanyula akizungumza wakati wa kumkaribisha Katibu Mkuu amesema kikao hicho kinawapa fursa wadau mbalimbali katika kuboresha Mwongozo huo ili wadau waweze kuutumia na kuongeza hamasa ya kuibua na kuendeleza wabunifu wa ngazi ya chini.

“Mkutano huu unajumuisha Wizara,Taasisi za Umma na hata zile za binafsi nazo tumeita wawakilishi ili tutajadili na kutengeneza huu Mwongozo ili kuchochea ubunifu,” amesema Prof. Kipanyula.

Naye Afisa Viwango kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mathias Nyaisanga amesema shirika hilo lipo kusaidia wabunifu kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.

Bw. Nyaisanga amebainisha kwamba kupitia uthibiti wa ubora wa bidhaa Shirika hilo linawasaidia wabunifu wachanga na wakubwa kufikia viwango na ubora wa bidhaa wanazozalisha.