Site icon A24TV News

WAZIRI MKUU MSTAAFU PINDA AFUNGUA MKUTANO WA PALU ARUSHA,ATOA UJUMBE MZITO

LMoses Mashalla,Arusha.

Waziri mkuu mstaafu nchini,Mizengo Pinda amefungua mkutano wa mawakili wa umoja wa Pan African (PALU) huku akisema kuwa suala la rushwa,ugaidi na utawala bora bado ni changamoto barani Afrika na kuutaka umoja huo kuhakikisha wanakemea vikali changamoto hizo.

Pinda,alitoa kauli hiyo jana katika mkutano huo unaowakutanisha mawakili mbalimbali barani Afrika huku akisema kuwa changamoto ya vita vya mara kwa mara katika baadhi ya nchi barani Afrika zimesababisha matatatizo ya kiuchumi na kupelekea bara la Afrika kuendelea kuwa maskini.

Waziri mkuu huyo mstaafu aliwataka washiriki katika mkutano huo kuhakikisha wanazingatia ajenda ya umoja wa Afrika ya 2063 kwa kuhakikisha Afrika inakuwa sehemu salama kwa uwekezaji ili kutokomeza suala la umaskini.

Hatahivyo,Rais wa umoja huo Emeka Ebegolu,aliutaka Umoja wa Afrika(AU) kuhakikisha wanasimamia sheria za uhuru wa habari barani Afrika na kukemea baadhi ya nchi zinazokandamiza uhuru huo. 

Alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa nchi barani Afrika hawazingatii utawala wa sheria kwa kuongeza muda madarakani kinyume na sheria na kuwataka viongozi hao kuheshimu dhana ya utawala bora.

Alisisitiza kwamba baadhi ya nchi barani Afrika uchumi wao umedorora kutokana na viongozi wake kutoheshimu dhana ya utawala bora na kusisitiza kuwa ni muda sasa Afrika kukemea na kuchukua hatua kutokomeza changamoto hiyo.

Naye katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),Peter Mathuki alizitaka nchi mbalimbali barani Afrika kuhakikisha wanazingatia suala la utawala bora wa kisheria ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.

“Ninatoa wito kwa viongozi mbalimbali barani Afrika kuhakikisha wanafuata misingi ya utawala bora wa kisheria ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara ” alisema Mathuki.

Mathuki,alisema kwamba suala la kupanda kwa gharama za maisha kama mafuta barani Afrika kutokana na vita vya Rusia na Ukrain linapaswa kuwa fundisho kwa bara la Afrika kuepuka utegemezi na kuanza kujitegemea.

Mwisho..