Serikali inatarajia kufanya marekebisho kwenye sheria ya mifumo ya malipo ya Taifa kwa kupunguza tozo ya muamala wa huduma za fedha katika simu za viganjani.
Hayo yamesemwa bungeni leo Jumanne Juni 14, 2022 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akisoma hatuba ya mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Akisoma kipengere cha sheria ya mifumo ya malipo ya taifa, Dk Mwigulu amependekeza kufanya marekebisho kwenye mfumo huo.
“Napendekeza kupunguza tozo ya muamala kutoka kiwango kisichozidi Sh7, 000 hadi kiwango kisichozidi Sh4,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa.
“Punguzo hili ni sawa na asilimia 43 ya kiwango cha sasa. Sambamba na hilo, napendekeza kuongeza wigo wa tozo hiyo ili kuhusisha miamala yote ya kielektroniki. Lengo la hatua hii ni kupunguza makali ya maisha kwa Mtanzania hasa katika kipindi hiki cha changamoto kubwa ya kiuchumi na kuweka usawa katika utozaji wa tozo hiyo,” amesema Dk Mwigulu.