Site icon A24TV News

ASKOFU HOTAY:-AFRIKA INA RASILIMALI NYINGI,IPUNGUZE MISAADA YA NJE.

Na Mwandishi wa A24Tv Arusha .

Askofu wa kanisa la Anglican Dayosisi ya Mt,Kilimanjaro,Stanley Hotay amesema ya kwamba Afrika ikiwemo Tanzania ina rasilimali za kutosha na kusema ni wakati wa kuwafundisha wananchi kujenga desturi ya kujitegemea.

Askofu Hotay alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya shirika la Here’s Life Africa Mission zilizofanyika katika kanisa hilo jijini Arusha.

Sherehe hizo ziliwajumuisha washirika wa makanisa ya kiinjili hapa nchini ,nchi za Afrika Mashariki ,kati pamoja na Afrika Magharibi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya sherehe hizo Askofu Hotay ambaye pia ni mkurugenzi wa shirika hilo alisema kuwa lazima waafrika ikiwemo Tanzania wafundishwe umuhimu wa kujitegemea katika kuendesha maisha yao badala ya kutegemea misaada kutoka nje ya nchi.

“Watu lazima waanze kujifunza kujitegemea tuna rasiliamali nyingi Afrika na Tanzania kwanini tusiwe sisi ndio tunatoa misaada bali kutarajia kwingine?watu wana uwezo wa kujitegemea na kuendesha maisha yao “alisema Askofu Hotay

Hatahivyo,alisisitiza kwamba katika miaka 25 shirika hilo limefanikiwa kuchimba visima vya maji safi na salama katika baadhi ya nchi za Afrika sanjari na kutoa elimu kuhusu ugonjwa hatari wa Ukimwi barani Afrika.

Naye mchungaji wa kanisa la Tanganyika African Church (TAC) wilayani Manyoni,Lazaro Mgonde alisema kuwa shirika hilo limemsaidia kukarabati jengo la kanisa analotumia ambalo lilitaka kubomoka.

“Shirika hilo limenitoa mbali sana maana kuna muda nilitaka kukimbia huduma lakini walinisaidia kuikarabati nyumba ya ibada ambayo ilitaka kubomoka “alisema Mgonde

Sara Guga ambaye ni mkurugenzi wa shirika la Jesus Glory alisema kuwa wamekuwa wakishirikiana na shirika hilo kuhubiri injili vijijini kupitia mahubiri ya sinema.

Guga alisema kuwa mbali na kuhubiri pia wamekuwa wakishirikiana kutoa huduma za kiafya kama upimaji wa macho na masikio ambapo wameyafikia maene mbalimbali nchini.

Mwisho..