Na Geofrey Stephen Arusha .
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Arusha(UOA) umejipanga kukusanya jumla ya kiasi cha sh,50 milioni kila mwezi kupitia programu ya “Book Project” Kama njia mojawapo ya kujikwamua na changamoto ya kifedha.
Mbali na programu hiyo pia kimeanzisha miradi mbalimbali ambayo ni ufugaji wa ng’ombe wa maziwa,kuoka mikate,kilimo cha mahindi,pilipili,maharage sanjari na duka kubwa la dawa za binadamu.
Chuo Hicho ni miongoni mwa vyuo vinavyomilikiwa na kanisa la Waadventista Wasabato nchini ambapo hivi karibuni kilizuiwa na serikali kudahili wanafunzi kutokana na sababu mbalimbali kabla ya kuruhusiwa kudahili wanafunzi mwishoni mwa mwaka huu .
Akizungumza na waandishi wa habari Naibu makamu mkuu wa chuo hicho kitengo cha mipango, fedha na utawala Prof Nkeni Pearson amesema kwamba Lengo kuu la mradi wa “Book Project” ni kukikwamua chuo chao na changamoto ya kifedha.
“Tunatarajia hadi kufikia mwezi Septemba kuanza mradi huu ambapo kila mwezi tunatarajia kukusanya milioni 50 hii programu itatusaidia kutukwamua na changamoto ya hali ya kifedha tunayopitia”alisema Prof Pearson
Hatahivyo,alisisitiza kuwa katika programu hiyo kila muumini wa kanisa la Waadventista nchini atachangia kiasi cha sh,1000 kwa mwezi kupitia nambari ambayo wataitoa hivi karibuni ambapo fedha watakazozikusanya zitawasaidia kulipa mishahara na kuongeza programu mpya.
“Tuliingia kwenye utawala wa chuo hiki wakati mgumu Sana kwani tulizuiwa kudahili wanafunzi lakini kupitia program hii tunatarajia kila mshirika wa kanisa la waadventista atachangia shilingi elfu moja kwa Mwezi ambayo itatuwezesha kulipa mishahara na kuongeza programu mpya”alisema Prof Nkeni
Alisema kwamba mbali na kuanzisha programu hiyo pia wanatarajia Kuanzisha kozi ya lugha mbalimbali ambayo ni kichina,kireno,kihispania na kihindi ambapo mitaala hiyo itasaidia kuongeza mapato ya chuo hicho.
Hatahivyo,mkuu wa chuo hicho,Prof Patrick Mano alisema kuwa wamejipanga katika kipindi cha miaka mitatu ijayo changamoto ya masuala ya kifedha ikiwemo mishahara ya watumishi itakuwa ni historia chuoni hapo.
Prof Mano ambaye ni raia wa Ghana alisema kuwa hapo awali alipokabidhiwa jukumu la kukisimamia chuo hicho fedha pekee waliyokuwa wakitegemea kuendesha chuo hicho ilitokana na makusanyo ya ada za wanafunzi ambayo haikidhi mahitaji lakini kwa sasa wameweka mikakati kukusanya fedha kupitia miradi mbalimbali.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa,kuoka mikate,mradi wa shamba la mahindi,maharage, pilipili ,parachichi sanjari na duka kubwa la dawa za binadamu.
“Nilipoingia hapa chuoni nilikuta fedha pekee wanayoitegemea kuendesha chuo ni ada za wanafunzi ambayo haitoshi endapo miradi hii ikifanikiwa vizuri suala la mahitaji ya wanafunzi na watumishi litakuwa limemalizika”alisema Prof Mano
Prof Mano aliomba ushirikino kwa wadau mbalimbali nchini na serikali kusaidia chuo hicho huku akisisitiza ya kwamba miongoni mwa changamoto kuu alizokutana nazo wakati anakabidhiwa majukumu ya kusimamia chuo hicho ni pamoja na masuala ya matumizi mabaya ya fedha za chuo sanjari na changamoto ya utawala bora ambayo kwa sasa imetatuliwa kwa asilimia 70.
Mwisho.