Moses Mashalla,
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Akheri ,Anael Nasari ameshauri watoto wafundishwe uungwana na maadili mema kuanzia ngazi ya familia ili kukomesha janga la mauaji nchini.
Hivi karibuni kumeripotiwa habari za mauaji ya mara kwa mara yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo mauaji yanayotokana na wivu wa kimapenzi.
Akizungumza katika ibada ya jumapili katika kanisa la KKKT usharika wa Akheri mchungaji Nasari alisema kwamba watoto wanapaswa kufundishwa maadili na uungwana tangu wakiwa wadogo ili wakikua wawe na tabia njema.
“Watoto wafundishwe maadili mema tangu wakiwa wadogo ni lazima uungwana uanzie katika ngazi ya familia “alisema Mchungaji Nasari
Hatahivyo,alisema kuwa matukio ya mauaji yanayoendelea nchini yanaakisi jamii iliyovurugwa na isiyostaarabika na kuitaka serikali ichukue hatua.
Mchungaji Nasari alisema kuwa ni lazima jamii ifuate ibada na malezi bora na kuondokana na ndoa za kubahatisha zisizofuata taratibu za mila,desturi na taratibu.
“Ndoa za kubahatisha hazifai tumekosa malezi ni lazima sasa tuheshimu mila,taratibu na sheria za ndoa lakini tuzingatie ibada “alisisitiza Mchungaji Nassari.
Mchungaji Nassari alimalizia kwa kuwataka walimu,wazazi,wanasiasa na jamii kwa ujumla kuacha kutumia lugha za matusi na kejeli ili kuepuka kujenga kizazi cha watoto wasio na maadili na heshima mbele ya jamii.
Mwisho…