Site icon A24TV News

KARANI WA SENSA AJIFUNGUA KABLA YA ZOEZI LA SENSA DC NASSARI AFUNGUKA ! KUHUSU ZOEZI LA SENSA BUNDA

Na mwandishi wa A24Tv .Musoma.

Karani wa Sensa ya Watu na Makazi wilayani Bunda mkoa wa Mara amejifungua muda mfupi kabla ya kuanza kazi hiyo, hivyo kulazimika kuondolewa kwenye orodha ya makarani katika wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari amesema kuwa karani huyo amejifungua usiku wa kuamkia Agosti 23, 2022 ingawa hakuweza kumtaja jina

“Tangu tumeanza tumepata changamoto ambayo pia ni baraka kuna karani wetu amejifungua usiku na bahati nzuri alijifungua kabla ya saa sita kwahiyo yeye na mtoto wake pia wamehesabiwa na baada ya hali hiyo kujitokeza tayari karani wa akiba ameshachukua nafasi na kazi inaendelea,” amesema Nassari.

Amefafanua kuwa wilaya ya Bunda inao makarani zaidi ya 1,000 na kwamba shughuli ya kuhesabu watu na makazi inaendelea na huku akiamini kuwa kazi hiyo itakamilika kwa ufanisi.

Amewataka wakazi wa Bunda kutoa ushirikiano kwa makarani na kutoa taarifa sahihi zitakazowiewezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa nchi na wananchi kwa ujumla.

Nassari pia amewataka wakazi wa wilaya hiyo hasa wale ambao bado hawajahesabiwa kuwa watulivu na wavumilivu kwa maelezo kuwa ni lazima kila mtanzania atahesabiwa katika muda ambao tayari umetangazwa.

“Nimekuwa nikipokea simu kutoka kwa watu wanalalamika kuwa bado hawajafikiwa naomba nitumie nafasi hii   kuwaondoa hofu kwamba lazima kila mtu atafikiwa, ndio kwanza siku ya kwanza imeisha,” amesema.

Amewataka wakuu wa kaya wilayani humo ambao bado hawajahesabiwa kuendelea na shughuli zao huku wakiwa wameacha taarifa zao na mawasiliano yao nyumbani ili makarani wakifika kwenye kaya zao iwe rahisi kupata taarifa zao.

Mwisho .