Na Geofrey Stephen Karatu .
Waziri wa Maji,Jumaa Aweso ametatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu wilayani Karatu baada ya kuamuru kuwepo kwa chombo kimoja kitakachosimamia utoaji wa huduma ya maji katika Mji huo huku akiagiza bei ya maji inayostahili kutozwa kwa sasa ni sh1,300 kwa uniti1 badala ya sh,2,000 hadi sh 3,000.
Aweso ameagiza kuungana kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Karatu (KARUWASA) na Mamlaka ya Utoaji wa Huduma ya Maji Vijijini (KAVIWASU) na kutengeneza chombo kimoja ambacho kitatoa huduma kwa wananchi kwa maslahi ya wananchi wa Karatu.
Hatahivyo waziri Aweso alitamka kwamba Rais Samia Hassan Suluhu ameridhia kutoa sh,bilioni 4.5 kwaajili ya mradi mkubwa wa maji wilaya hiyo na kuagiza mamlaka husika zianze kutangaza zabuni ya mkandarasi atakayetekeleza mradi wa kusambaza maji wilayani humo.
Awesso amesema hayo leo baada ya kusikiliza maoni ya wananchi na wadau mbalimbali wa maji wilayani humo ambapo awali kulikuwa na mgawanyiko wa maslahi ikiwemo Kaviwasu kutoza sh, uniti moja kwa sh,2000 hadi 3000 huku Karuwasa ikitoza sh,1,750 kwa bei za majumbani.
Alisema uwepo huo wa chombo kimoja kutawezesha maslahi ya wananchi ikiwemo utoaji wa huduma bora za utoaji maji pamoja na kuhakikisha miundombinu ya maji haiharibiki.
Alisema hakuna mtumishi yoyote atakayefukuzwa baada ya kuungana Karuwasa na Kaviwasa kwa kuwa watakapoungana lita zaidi ya milioni 6 zitakuwepo ndani ya mamlaka moja ambazo zitakidhi mahitaji ya wakazi wa wilaya hiyo.
“Wekeni utaratibu mkandarasi atangazwe aanze kazi ya kusambaza miundombinu ya maji na nyie wenyewe mtaunda bodi itakayopanga mipango yake kwani maji si biashara bali ni huduma,tuunganishe mamlaka hizi na utaratibu wa bei uwe ni sh,1300 kwa uniti 1 kwa kila mwananchi “alisema Aweso
Aliagiza bei atakayotozwa mwananchi wa kawaida kwa hivi sasa iwe ni sh,1,300 kwa uniti 1 wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji( Ewura) ikiendelea kuchakata bei halisi itakayotozwa kwa wananchi juu ya ulipaji wa ankara za maji.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba,alimshukuru Waziri Aweso kwa kutoa maagizo hayo kwani wananchi watanufaika na bei moja badala ya awali kuwa na mkanganyiko wa bei kati ya Karuwasa na Kaviwasu
Alisema baada ya Rais Samia kutangaza filamu ya Royal Tour watalii wamefurika wilayani Karatu na hivi sasa hoteli zaidi ya 60 zilizopo hapo zinahitaji maji hivyo aliomba wilaya hiyo kupewa zaidi vipaumbele vya maji ili kuwezesha kila mtu kunufaika na huduma za maji.
Awali,Ofisa Tawala Mkuu kutoka Wizara ya Maji,Jacob Kingazi akisoma mapendekezo ya kamati iliyoundwa na Waziri Aweso kwaajili ya kufanya tathimini ya hali ya upatikanaj wa huduma ya maji mji wa Karatu,alisema lazima kuwepo Kwa chombo kimoja kitakachosimamia utoaji wa huduma katika mji wa karatu ili kuondoa migogoro.
Kingazi alisema awali walibaini bodi kuendelea kutekeleza baadhi ya majukumu ya kiutendaji ilhali ilifikia ukomo mwaka 2019 ikiwemo ukusanyaji wa ukusanyaji mapato.
Naye mbunge la jimbo la Karatu, Daniel Awackii alimshukuru Waziri,Aweso kwa kuunganisha bodi hizo mbili na kuwa moja kwaajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi na kuongeza kuwa hivi sasa watafanya vikao kwa wanachi kwaajili ya kuwaeleza wananchi kulipa ya bei hiyo ya unit 1,300 kwa kila mmoja badala ya sh,2000 hadi 3000 zinazotozwa na Kaviwasu
Mwisho.