Site icon A24TV News

MAIPAC na CILAO yabaini utajiri wa maarifa ya asili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kutunza Mazingira

Mwandishi wetu, Arusha

Shirika la wanahabari la kusaidia jamii za Pembezoni (MAIPAC) na shirika la msaada wa kisheria na elimu ya Uraia(CILAO) yamebaini utajiri wa maarifa ya asili ambao unaweza kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Wakizungumza katika kikao cha kupitia na kuhakiki taarifa za uchunguzi zilizokusanywa katika wilaya za Longido, Ngorongoro na Monduli kupitipia mradi wa ukusanyaji maarifa ya asili katika utunzwaji Mazingira,Vyanzo vya maji na kukabiliana na changamoto na mabadiliko ya tabia wakurugenzi wa mashirika hayo walibainisha ni muhimu sana maarifa ya asili kutunzwa na kuendelezwa.

Walisema kupitia mradi huo ambao udhamini wa na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa(UNDP) kupitia mfuko wa mazingira Duniani(GEF) na kuratibiwa na jumuiko la maliasili Tanzania(TNRF) utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na watungaji wa sera.

Mkurugenzi MAIPAC Mussa Juma na Mkurugenzi wa shirika la CILAO, Odero charles Oderos, walieleza katika mradi huo wamefika katika wilaya tatu za Monduli, Longido na Ngorongoro na na timu za wanahabari kukutana na makundi ya wazee maarufu, viongozi wa mila, wanawake, vijana na wanafunzi na kukusanya maarifa za asili katika masuala ya mazingir

Juma alisema jamii za pembezoni zina utajiri mkubwa wa maarifa ya asili lakini, kama yasipohifadhiwa yanaendelea kutoweka na hivyo, jamii kutegemea elimu za kisasa pekee katika utunzwaji wa mazingira.

Kwa upande wake Odero alifafanua kuwa, maarifa ya asili ambayo yatakusanywa katika mradi huo, yatawekwa katika vitabu na kwenye vyombo vya habari ili kuzalia kutumika katika utungaji wa sera lakini pia kuelimisha jamii umuhimu wa maarifa hayo.

Afisa misitu wa tarafa ya Makuyuni na Manyara, Hapiness Masaki na Afisa misitu wa Wakala wa misitu(TFS) wilaya ya Ngorongoro, Major Ngoilenya walisema ni muhimu maarifa ya asili kutumika katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi katika kutunza vyanzo vya maji na misitu.

Afisa Mifugo na mabadiliko ya tabia nchi wilaya ya Longido,Nestory Daqqaro alisema katika kipindi cha miezi tisa,wanyama takribani 38,720 wamekufa wakiwepo Twiga wanne, Pundamilia 18,Swala 2 na wengine ni Ng’ombe, kondoo na mbuzi .

” jitihada zinaendelea kufanywa hapa wilayani ikiwepo kuchimba visima na kupeleka maji maeneo ya wanyama, kutenga malisho ili kuokoa maisha ya wanyama na uchumi wa wilaya hiyo, ambapo asilimia 95 ya wananchi hutegemea mifugo”alisema

Mkurugenzi wa jumuiko la Maliasili Tanzania(TNRF), Zakaria Faustine akizungumza katika mkutano huo, alisema kuna haja kuwa na mkakati shirikishi baina ya asasi za kiraia, serikali, mashirika ya kimataifa na wananchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Faustine alisema mradi wa kukusanya maarifa ya asili yanayoweza kutumika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kutunza misitu na maji ambao unatekelezwa na MAIPAC ni sehemu ya mkakati wa kupata taarifa ili kusaidia maboresho ya sera na sheria nchini.

“tunawapongeza MAIPAC na CILAO kwa mradi huu, ambao unatekelezwa pamoja na miradi mingine 12 ya mazingira ambayo inafadhiliwa na UNDP kupitia programu ya miradi midogomidogo kwa lengo na kushirikisha jamii za asili katika utunzwaji wa mazingira na vyanzo vya maji”alisema

Mwenyekiti wa kijiji cha Kimokowa, wilaya ya Longido, Kilei Mollel alisema licha ya wilaya hiyo, kukabiliana na ukame na kukosa maji pia imeibuka mimea vamizi ambayo hailiwi na mifugo na wanyamapori ambayo imeota katika maeneo mengi.

“tumekuwa tukishirikiana na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kama CORDs kung’oa mimea lakini ni mingi zaidi ya hekali 1000 za malisho zimevamiwa”alisema
.
Mkurugenzi wa shirika la MIMUTIE women Orgganization (MWO) Rose Njilo akizungumza katika mkutano huo, licha ya kupongeza mradi wa kukusanya taarifa za maarifa ya asili unaotekelezwa na shirika la MAIPAC, alisema hivi sasa wanaoathirika na mabadiliko ya tabia nchi ni wanawake na watoto.

“mradi huu umekuja wakati muafaka sasa elimu ya asili itambulike na watunga sera ili iweze kuwasaidia wanawake na watoto jamii za pembezoni ambao ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi”alisema

Afisa habari wa shirika la PINGOs Forums, Elie Chansa alitaka taarifa za asili ambazo zitakusanywa katika mradi huo,zifikishwe serikalini na katika mashule na vyuo ili ziweze kutumika katika kutunza mazingira kabla walivyofanya mababu.

Mradi wa kukusanya taarifa za uhifadhi mazingira, kutunza vyanzo vya maji, misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, unatekelezwa na shirika la MAIPAC kwa kushirikiana na shirika la CILAO katika wilaya tatu za mkoa Arusha ambazo ni Longido, Monduli na Ngorongoro.

MWISHO