Site icon A24TV News

NAIBU KATIBU MKUU WA UWEKEZAJI ATEMBELEA BANDA LA TUME YA MADINI KWENYE MAONESHO YA MADINI GEITA

Na Mwadishi wa A24Tv Geita .

Naibu Katibu Mkuu Uwekezaji kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ally Gugu amefanya ziara kwenye Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Ukanda wa Uwekezaji (EPZ) Bombambili, mkoani Geita.

Mara baada ya kupata maelezo kutoka kwa wataalam, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Madini na Tume ya Madini na kuongeza kuwa Wizara yake ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Madini na Taasisi zake kwenye eneo la uwekezaji ili kuhakikisha wawekezaji wengi wanawekeza kwenye Sekta ya Madini.

“Sisi kama Wizara inayoshughulikia uwekezaji tupo tayari kuendelea kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini hasa kwenye eneo la madini ili wananchi waendelee kunufaika na rasilimali za madini huku uchumi ukiendelea kukua,” amesema Gugu.

Maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu ya “Madini ni Fursa za Uchumi, Ajira kwa Maendeleo Endelevu”, yamejumuisha pia washiriki kutoka mataifa mbalimbali kutoka Afrika ikiwa ni pamoja na Zambia, Uganda na Burundi.