Site icon A24TV News

RAIS SAMIA AWEKA HISTORIA UJENZI WA HOSPITALI YA MAMA NA MTOTO LUSHOTO DC TUMESIMAMIA ILANI

Na Geofrey Stephen . Lushoto

AKINA MAMA zaidi ya 250,000 katika Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga wanatarajia kuondokana na changamoto ya vifo vya watoto wachanga baada
ya serikali kujenga hospitali ya kubwa ya kisasa ya mama na mtoto yenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.3

Muonekano wa Jengo la Kisasa la  Hospital ya Mama na Mtoto 

Akiongea na vyombo vya habari katika ziara yake ya  kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali wilayani humo ikiwemo  hospitali hiyo,

Mkuu wa Wilaya hiyo,Kalisti Lazaro alisema kuwa mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na kukamilika kwake kutaondoa changamoto ya vifo vya mama na mtoto  .
Kalist Lazaro Mkuu wa wilaya ya Lushoto Akizungumza katika Hospitali ya Mama na Mtoto

Mkuu huyo wa wilaya ambaye ametimiza mwaka mmoja na nusu wa uongozi wake wilayani humo ,alisema kuwa wilaya hiyo haikuwa na hospitali ya mama na mtoto lakini anaishukuru serikali ya awamu ya sita,Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wa wilaya ya Lushoto hususani kwa
kujenga hospital hiyo yenye ghorofa moja.

Alisema kukamilika kwa hospital hiyo kunaweza kusaidia wananchi wa Miji ya Mombo Wilayani Korogwe na wananchi wa Mji wa Same waliopo katika wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro hivyo jitihada za ziada
zinahitajika ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati ifikapo desemba mwaka huu.

Mganga Mkuu wa Hospitali Ya wilaya Lushoto Akizungumzia Mradi Huo Kwa Vyombo Vya Habari

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Lushoto {DMO} ,Godfrey Andwer amesema kuwa hadi sasa jengo hilo limegharimu zaidi ya shilingi milioni 837 na linatarajia kukamilika desemba mwaka huu.

Alisema jengo likikamilika linatakiwa kuwa na vifaa vyote vya kisasa vya upasuaji na huduma nyingine kwani MSD imeahidi kutoa vifaa vya zaidi ya shilingi milioni 110 vya hospital hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Chama        Cha Mapinduzi{CCM} Wilaya ya Lushoto,Ally Daffa amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya afya,elimu,maji,umeme na
barabara imetekelezwa kwa asilimia kubwa ikiwea ni moja ya utekelezaji wa ilani ya chama.

Daffa alisema na kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Lushoto kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa miradi na kuwataka wananchi
kuhakikisha wanailinda miradi hiyo kwa gharama zote.

Mwenyekiti wa Chama  Cha Mapinduzi{CCM} Wilaya ya Lushoto,Ally Daffa.
Alisema jukumu ;la kulinda miradi ni la kila mwananchi wa wilaya ya Lushoto na sio jukumu hilo la watu pekee kwani faida ya miradi hiyo ni kwa wananchi wote wa wilaya hiyo na sio vinginevyo.
Mwenyekiti huyo alisema na kuwataka watendaji wa halmashauri za lushoto na Bumbuli kuhakikisha wanakuwa watiifu na waaminifu wa fedha
za miradi ya serikali vinginevyo dola haitawaacha salama.Mwisho.