Site icon A24TV News

TUME YA MADINI YAENDELEA KUIPAISHA SEKTA YA MADINI

Na Mwandishi wa A24tv

_Ni kupitia kasi ya utoaji wa leseni za madini 9,498 mwaka 2021-2022_

_Uanzishwaji wa masoko 42 na vituo vya ununuzi wa madini 83_

_Leseni za madini 9,498 zatolewa mwaka 2021-2022_

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume, Sekta ya Madini imeendelea kuimarika kutokana na mafanikio yaliyopatikana ndani ya muda mfupi ikiwa ni pamoja na kasi ya ukusanyaji wa maduhuli, uanzishwaji wa masoko na vituo  vya ununuzi wa madini nchini na utoaji wa leseni za madini.

Profesa Kikula ameyasema hayo leo Oktoba 11, 2022 jijini Mwanza  kwenye kikao cha Tume ya Madini kilichoshirikisha Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba, Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa chenye lengo la kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi hasa kwenye eneo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2022-2023, usimamizi wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini, usimamizi wa mazingira na afya kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini na namna watanzania wanavyoweza kunufaika kupitia Sekta ya Madini.

Ameeleza mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Tume kuwa ni pamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa maduhuli kutoka shilingi bilioni 346.78 kwa kipindi cha mwaka 2018-2019 hadi kufikia shilingi bilioni 624.61 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021-2022 ikiwa ni sawa na asilimia 96.09 ya lengo la mwaka husika.

Profesa Kikula ameendelea kueleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko 42 na vituo vya ununuzi wa madini 83 na ongezeko la utoaji wa leseni za madini ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021-2022 Tume ilitoa jumla ya leseni za madini 9,498 ikilinganishwa na leseni 6,314 zilizotolewa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020-2021.

Aidha, Profesa Kikula amesema kuwa ili kusogeza huduma karibu zaidi na wadau wa madini, Tume ilianzisha ofisi mpya za madini katika mikoa ya Mbogwe na Mahenge.

Ameendelea kusema kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua kutoka asilimia 4.8 katika kipindi cha mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 7.2 katika kipindi cha mwaka 2021.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa ili kuhakikisha lengo lililowekwa na Serikali la kukusanya  kiasi cha shilingi bilioni 822 kwa mwaka wa fedha 2022-2023 linavukwa.

“Serikali na wananchi kwa ujumla wana matarajio makubwa kwenye Sekta ya Madini na sisi kama Tume ya Madini ni vyema tukajipanga katika kuhakikisha tunakidhi matarajio huku kila mtanzania akinufaika na Sekta ya Madini,” amesema Profesa Kikula.

Aidha, Profesa Kikula amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akizungumza katika kikao hicho, amewataka viongozi wa Tume kuendelea kuimarisha mshikamano na kufanya kazi kama timu moja ili kuweza kufikia malengo ya Tume ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini

Aidha, Mhandisi Samamba ameshukuru kwa ushirikiano ulioendelea kutolewa na viongozi wa Tume, hivyo mafanikio kuendelea kuonekana kila mwaka.