Site icon A24TV News

WIKI YA HUDUMA YA FEDHA KITAIFA KUFANYIKA JIJINI MWANZA NOVEMBA 21MPAKA 26 MWAKA HUU.

Na Doreen Aloyce, Dodoma

Katika kuelekea wiki ya huduma ya fedha inayotarajia kufanyika Novemba 21 mpaka 26 Jijini Mwanza mwaka huu, Wizara ya Fedha imejipanga kujenga uelewa na weledi kwa Umma juu ya uelewa wa fedha ambapo imesema mpaka sasa asilimia 40 ya idadi ya watanzania waishio vijijini hawajafikiwa

Aidha katika utekelezaji wa Program ya utoaji Elimu wa masuala ya Fedha Serikali inakusudia ifikapo mwaka 2025 takribani asilimia 80 ya wananchi watakuwa wamepata uelewa wa masuala ya Fedha.
Akizungumza Jijini Dodoma alipokuwa akitoa maelekezo kuhusu wiki ya huduma ya Fedha kitaifa Kamishna uendeshaji wa sekta ya Fedha Charles Mwamwaja kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara alisema kuwa Kutokana na Utafiti wa FinScop wa mwaka 2017 Nchini ni asilimia 48.6 tu ya nguvu kazi ndiyo waliotumia huduma rasmi za fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizo.

“Hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuchangia katika kukuza Pato la Taifa,”alisema.

Aidha alieleza kuwa malengo ya wiki ya huduma za fedha ni pamoja na kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini.

Na Kuimarisha ufanisi wa masoko ya Fedha kupitia elimu ya Fedha,kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha,kutoa elimu ya kuwezesha kumlinda mtumiaji wa huduma za kifedha,kuwezesha wananchi kusimamia vizuri Rasilimali fedha.

“Kuwezesha wajasiriamali wadogo kuongeza ujuzi na matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao,kuimarika kwa Utamaduni wa kujiwekea akiba,kukopa na kulipa madeni pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya Fedha kwenye ukuaji wa uchimi,”alisema.

Aidha alisema kuwa wiki ya huduma za fedha inalenga kuwafikia wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma, wanafunzi,wakufunzi,wanawake,vijana,watu wenye mahitaji maalum,wajasiriamali wadogo na wakati(SMEs),asasi za kiraia,wahariri na waandishi wa vyombo vya habari,watoa huduma za fedha,watoto na ummakwa ujumla.

Maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa ni utekelezaji wa Mpango mkuu wa mendeleo ya sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21-2029/30,elimu kwa umma ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango huo.

Wizara ya fedha na Mpango imeandaa programu ya kutoa elimu kwa umma ya mwaka 2021/22-2025/26 programu hiyo imeweka mikakati ikiwa ni pamoja na matukio na mbinu mbalimbali zitakazotumika katika utoaji wa elimu ya Fedha kwa umma.

Mwisho.