Rai imetolewa kwa walimu wote wa shule za msingi na sekondari na vyuo nchini kupunguza matumizi ya viboko na vitisho kwa wanafunzi kama njia ya kufanya wafaulu katika masomo yao kwa kuwa huo si mtazamo sahihi.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa wadau wa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) ambapo alimwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael.
Ameongeza kuwa walimu wanatakiwa wafahamu kuwa watoto wote hawana uwezo unaofanana hivyo wanatakiwa kuwachukulia watafute mbinu mbalimbali za kumsaidia kila mmoja.
“Maendeleo ya kweli katika nchi huletwa na elimu bora, elimu bora huletwa na walimu bora na walimu bora sifa yao kuu ni upendo kwa wanafunzi na wadau wengine wa elimu. Mwalimu ni kioo cha jamii, amejaa hekima na busara na ni kimbilio la watu wote,” amesema Dkt. Mtahabwa.
Amesema lengo la mkutano huo ni kutafakari namna ambavyo mradi umekuwa ukitekelezwa na kujadili jinsi ya kuimarisha na kuendeleza mambo yaliyotekelezwa kwa mafanikio baada ya mradi kuisha.
“Kwa hiyo siku hizi mbili tutaangalia nini kimefanyika kupitia Mradi huu wa TESP na kisha kuweka mikakati ya namna ya kuendeleza mradi huu,” ameongeza Dkt. Lyabwene.
Mratibu wa Mradi wa TESP, Cosmas Mahenge amesema mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Canada umejikita katika kuimarisha elimu ya ualimu, hasa katika ngazi ya Astashahada na Stashahada za Ualimu katika Vyuo vya Ualimu vya Serikali na kwamba una jumla ya zaidi ya Shilingi bilioni 90.
Ametaja kazi kubwa zilizofanywa na mradi huo kuwa ni kutoa mafunzo kwa Wakufunzi zaidi ya 1,300, kununua vifaa vya TEHAMA kwa vyuo vyote 35 vya umma na kuviunganisha katika mkongo wa taifa wa mtandao.
Nyingine ni ujenzi wa Chuo cha mfano cha Ualimu Kabanga, ujenzi na ukarabati katika vyuo saba, kukarabati na kujenga maktaba za kisasa, maabara za Tehama na za sayansi, kuimarisha uongozi kwa kuwapa mafunzo ya uongozi kwa viongozi na maafisa Wizara ya Elimu Makao Makuu lengo likiwa kuimarisha mfumo wa kusimamia elimu ya ualimu.
Naye Mwenyekiti wa Wakuu wa vyuo vya Serikali, Tanzania Bara Agustine Sahili amesema wamenufaika na mradi huo kwa kupata mafunzo kwa wakufunzi wa vyuo vyote
Ameongeza kuwa manufaa mengine waliyopata ni vyuo kujengewa na kukarabatiwa miundombinu ikiwemo maktaba mpya na maabara za Tehama na za sayansi.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Canada, Rasmatta Barry ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa utekelezaji wa mradi huo ambao amesema umezingatia masuala ya mazingira na jinsia kwa kiasi kikubwa.