Site icon A24TV News

Balozi Njoolay Aiasa CCM kuwa Wamoja

Na  Geofrey Stephen .Arusha

Balozi Mstaafu,Daniel Ole Njoolay amesema  wakati umefika wa Chama Cha Mapinduzi[CCM] kujisafisha na kujirekebisha kasoro zote ili chama hicho kiwe kitu kimoja kwa maslahi ya Nchi.

 

Njoolay alisema hayo leo Jijini Arusha wakati akiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha,Stephen Zellothe na viongozi mbalimbali wa Chama wakitoa kauli ya Mkoa juu ya kuruhusiwa kwa vyama vya siasa kufanya Mikutano ya hadhara,marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa na marekebisho ya katiba iliyotolewa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Alisema iwapo CCM itakuwa kitu kimoja vyama vya siasa hawatakuwa naa hoja katika Mikutano yao ya hadhara na kama hilo halitakuwepo vyama vya siasa vitapata mwanya wa mgawanyiko ndani ya chama kushambulia chama tawala.

Balozi aliwataka wana CCM wote kote Nchini kuwa kitu kimoja na kujikita katika kuisimamia serikali kuhakikisha inatekeleza miradi yote ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi.

Alisema Rais kuondoa zuio la Mikutano ya hadhara ni jambo jema sana na linapaswa kupongezwa kwa dhati kwani Rais amedhubutu na ametumia uzalendo wenye lengo la kujenga Nchi.

Balozi Njoolay alisema Nchi hii ni ya kila mwananchi wa Kitanzania hivyo kila mmoja anawajibu wa kuijenga kwa kufuata sheria na kanuni zilizoko na Nchi hii sio ya Chama tawala pekee yake.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha ,Stephen Zellothe alisema kuwa uamuzi wa Rais uliofanywa juzi ni wenye busara,hekima na uzalendo kwa maslahi ya Nchi hivyo anastahili kupongezwa na kuungwa mkono kuwa Rais Tena katika awamu ijayo.

Zellothe alisema Mkoa wa Arusha ulitengewa shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama vile elimu,maji,barabara na afya na tayari madarasa 268 yamejengwa kwa ajili ya wanafunzi wa kidatu cha kwanza na wanafunzi wote wataingia darasani.

Alisema na kuvitaka vyama vya siasa kuacha siasa za chuki na zenye kubomoa Nchi kwani sio siasa za watanzania kwani siasa za sasa zinapaswa kujikita katika kuijenga Nchi kwani wote wanajenga nyumba moja na haina haja ya kugombani vito.

‘’Siasa zinapaswa kufanywa kiustarabu,kiungwana na zenye hoja lengo ni kujenga Nchi kwani wote tunajenga nyumba moja haina haja ya kugombania vito’’alisema Zellothe

Mwenyekiti alisema hakuna kiongozi asiyekuwa na mapungufu ila mapungufu yanapaswa kuelezwa kwa staa kwa kuzingatia maadili ya Nchi kwani watanzania hawajazoea lugha za matusi,kejeli na udhalilishaji kwa kufanya hivyo ni kukiuka maadili yaliyoachwa na waasisi kwani waliacha Nchi katika maadili mema yenye kufuata misingi ya haki za binadamu.

Alisema CCM iko kwa ajili ya kuisimamia serikali ikiwa ni pamoja na kuhakikishaa miradi yote ya maendeleo inajengwa kwa kiwango cha hali ya juu na kuhakikisha thamani ya fedha inakuwa kama ilivyokusudiwa katika miradi yote na sio vinginevyo.

Zellothe aliwataka wana CCM Mkoani Arusha kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kuisemea serikali katika utekelezaji wa miradi yote ya Maendeleo katika maeneo yao ili wapinzani wasiwayumboishe wananchi.

Mwisho.