Site icon A24TV News

KANISA LA KKAM ARUSHA ,LAPIGA VITA UKATILI,IBADA YA KUKARIBISHA MWAKA MPYA2023

Doreen Aloyce, Arusha.

Wazazi kote nchini wametakiwa kuanza mwaka mpya wa 2023 kwa kuwa makini na watoto wao hasa wanapotoka shule kuwadhibiti katika matumizi ya simu za kiganjani ili kujenga kizazi kilicho bora.

Hayo yamesemwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la KilutherI Afrika Mashariki(KKAM) Tanzania Oscar Olotu kwenye Ibada ya kuukaribisha mwaka mpya 2023 iliyofanyika katika Kanisa la Kilutheri la Afrika Mashariki lililopo Kwangulelo jijini Arusha.

Askofu Olotu amesema kuwa watoto wengi wa siku hizi wamekuwa wajanja na mitandao ya kijamii kwa kutumia simu jambo linalopelekea kuangalia video ambazo hazina maadili kwenye jamii.

“Niwatake wazazi tunapoanza mwaka huu wazazi muendelee kuwa makini na watoto kuhusu mienendo yao wanapoenda na kutoka shuleni kujua makundi waliyonayo hii itasaidia kuwa na makuzi mema kimaadili” amesema Askofu Olotu.

Katika hatua nyingine amewataka watanzania kutunza mazingira yanayowazunguka hasa kupanda miti hali itakayopelekea kuwa na hewa safi na kupata mvua ya kutosha.

“Niwatake wakristo wenzangu tujitahid kutunza mazingira yetu tusikate miti hovyo kwa kutengenezea mkaa inapalekea kupotea mvua na viumbe hai” amesema Askofu Olotu.

Kwa upande wake Askofu wa kanisa hilo katika jimbo la Arusha Dkt.Philemon Mollel amewataka waumini kuhakikisha kanisa linakuwa sehemu salama ya kujenga jamii yenye maadili mazuri.

Nao wakristo kaunda Mollel Erick Jeremiah, wameeleza jinsi mmomonyoko wa maadili unavyoshika kasi katika jamii na kuahidi kusimamia maelekezo ya viongozi wao wa kiroho ya kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili mema.

Mwisho.