Site icon A24TV News

TFRA YAFUTA LESENI YA WAKALA WA MBOLEA NJOMBE

Na Emmanuel Njombe .

Mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania TFRA imetangaza kufuta leseni ya wakala wa mbolea aliyekamatwa akitakatisha mbolea mkoani Njombe na kuwauzia wakulima kinyume Cha sheria.

Akitangaza hatua hiyo mkurugenzi wa mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania TFRA Dokta Stephan Ngailo baada ya kuzulu mkoani Njombe na kushuhudia nyumba nyingine ya mfanyabiashara huyo iliyopo mtaa wa Kwivaha mjini Njombe ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kuhamishia mbolea zinazochakachuliwa amesema licha ya kufuta leseni hiyo lakini anapaswa kushtakiwa kwa tuhuma anazokabiliwa nazo.

 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa amesema hadi sasa zaidi ya watu 10 wanashikiliwa na jeshi la Polisi kutokana na sakata hilo wakiwemo waliokuwa wakihusika kusafirisha mifuko,mashine za kufungashia mifuko pamoja na wauzaji wa mbolea hizo kwenye maduka.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka amewataka wananchi kutoa taarifa kwenye mamlaka za serikali pindi wanapobaini kuwapo kwa utofauti wa mbolea wanazonunua huku akilipongeza jeshi la polisi kwa kufanikisha upatikanaji na ukamataji wa watuhumiwa hao.

Aidha Mtaka amesema kama sio uzalendo na weledi wa jeshi la polisi mkoa wa Njombe wangeweza kuingia makubaliano ya kilaghai na mfanyabiashara huyo ili wasitoe taarifa juu ya uwepo wa utakatishaji mbolea hizo.

Tayari serikali ilishayafunga maduka ya mfanyabiashara huyo wa mbolea ambaye jina lake limehifadhiwa kutokana na kuhusika kuchakachua mbolea hizo na kuziuza kwa mfumo wa Ruzuku ya serikali katika mtaa wa Mgodechi na Kwivaha mjini Njombe.

Mwisho .