Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo amewataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa umahiri, weledi na ubunifu ili malengo ya sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yaweze kufikiwa.
Prof. Nombo ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa mapokezi yake na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula baada ya kuteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amesema Wizara hiyo imepewa majukumu makubwa ya kuhakikisha elimu inayotolewa kwa Watanzania inakuwa bora na kuimarisha Sekta ya Sayansi na Teknolojia.
Ameongeza hivi sasa Wizara ipo katika hatua za mwisho za kuhuisha Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Mitaala, huku akisisitiza kuwa si Tanzania pekee inayofanya mageuzi hayo bali Dunia nzima ipo katika kufanya mageuzi ya elimu.
“Mageuzi katika utendaji kwa kufanya kazi kwa weledi, umahiri, ubunifu na uwazi ni muhimu ili kufikia yale mageuzi tunayoyatamani katika sekta ya elimu,” amesisitiza Katibu Mkuu.
Prof. Nombo amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaamini na kumpa nafasi katika utumishi huo.
Aidha amewashukuru Makatibu Wakuu waliotangulia kwa kuweka misingi imara katika kuelekea mageuzi nchini.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Franklin Rwezimula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kutumikia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa watumishi ili kuendelea kuboresha sekta ya elimu.