Site icon A24TV News

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kuzoa taka ya Together We Can Do Women Group ya Jijini amefikishwa Mahakamani kwa kushindwa kulipa shilingi milioni 49.9 za Jiji hilo.

Na Geofrey  Stephen,Arusha

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kuzoa taka na Usafi wa Mazingira ya Together We Can Do Women Group ya Jijini Arusha,Neema Mosha{39} mkazi wa kata ya Moshono Mtaa wa Moshono Kati amefikishwa Mahakamani kwa tuhuma kushindwa kuwasilisha shilingi milioni 49.9 za Jiji hilo.

Akisomewa mashitaka hayo leo na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa{TAKUKURU} Mkoani Arusha,Rubein Maduhu ilidaiwa kuwa Mosha alitenda kosa hilo katika kipindi cha mwaka 2021/22 wakati Kampuni hiyo ilipopewa Uwakala wa kazi hiyo ya kuzoa taka na usafi wa Mazingira.

Maduhu alidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Arusha,Regina Oyeri na kudai kuwa mtuhumiwa Mosha alitenda makosa hayo wakati akijua wazi kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Mwendesha Mashitaka wa Takukuru alisema kuwa dhamana ya shitaka hilo iko wazi kwa mtuhumiwa kwa kuwa shitaka hilo liko wazi kisheria kudhaminiwa na mtuhumiwa alikidhi vigezo akiomba Mahakama kutoa dhamana ya watu wawili wenye mali isiyohamishika yenye thamani ya kosa analoshitakiwa nalo Mosha.

Hata hivyo Mwendesha Mashitaka huyo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo alimwomba Hakimu kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo.

Hakimu Oyeri alipanga usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo kufanyika march 13 mwaka huu katika Mahakama hiyo na mtuhumiwa alitakiwa kufika bila ya kukosa.

Mwisho