Na Geofrey Stephen Arusha
RUFAA YA wananchi wa vijiji vinne vya kata Ololosokwan kwenye tarafa ya Loliondo wametinga kwenye Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki, (EACJ) mbele ya majaji watano wakiongozwa na Rais wa mahakama hiyo, jaji, Nestor Kayobera ambapo kuna mambo manne yanayobishaniwa.
Rufaa hiyo imefika mahakamani hapo leo Februari 6, 2023 kwa ajili ya kupangiwa utaratibu wa kusikilizwa ambapo mahakama hiyo imewataka mawakili wa waleta rufaa kuwasilisha hoja zao za rufaa za maandishi ndani ya siku 30 mpaka Machi 6, 2023.
Mawakili wa mjibu maombi ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, (AG) wametakiwa kuwasilisha hoja zao majibu ndani ya siku 30 mpaka Aprili 5,2023 na endapo waleta maombi watakuwa na hoja za nyongeza waziwasilishe ndani ya siku 14 mpaka Aprili 19, 2023.
Baada ya hapo Msajili wa mahakama atawapa mawakili wa pande zote taarifa ya tarehe ya usikilizwaji wa shauri hilo ambapo kika upande watakuwa na dakika 30 za kuwasilisha mambo ya muhimu yaliyo kwenye hoja zao.
Hoja za wananchi hao kwenye rufaa hiyo namba 13/2022 o zimewasilishwa na mawakili wao Donald Deya, Esther Muiga-Mnaro, Jebra Kambole, Praisegod Joseph Oleshangay.
Mambo yanayobishaniwa kwenye rufaa hiyo ni ile ambayo wananchi hao wanadai mahakama ya awali haikufuatilia vizuri ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi wa waleta rufaa.
“Ushahidi wa watu wengi, wanawake , wanaume, vijana na watu wazima uliwasilishwa mahakamani ambao tukiangalia kumbukumbu ya mahakama ya awali haikuuzingatia,” amesema wakili Deya ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Chama Cha wanasheria Barani Afrika,(PALU) na kuongeza.
“Katika ushahidi tuliotoa (kwenye mahakama ya mwanzo ya (EACJ) ulionyesha dhahiri ukiukwaji wa haki za binadamu lakini mahakama ya mwanzo haikuipa uzito unaostahili,”.
“Hawakuangalia ushahidi wetu kisheria kwa vile viwango vya kisheria vinavyoelekeza kwani wangefanya hivyo hukumu ingekuwa sawa kisheria,”.
Mawakili hao wa waleta maombi wameiomba mahakama ya rufaa iyapitie upya hoja zao kisha watoe hukumu inayostahili kwa mujibu wa sheria.
Majaji wengine waliosikiliza upangaji wa usikilizwaji wa shauri hilo ni pamoja na Makamu wa Rais wa EACJ, Sauda Mjasiri, Anita Mugeni, Kathurima M’Inoti na Cheborion Brishaki.
Mwanasheria mkuu kwenye shauri hilo anawakilishwa na mawakili wa serikali, Vivian Method na Narindwa Sekimanga.
Awali septemba 20,2022 mahakama ya mwanzo ya EACJ ilitupilia mbali maombi ya wananchi hao kwa kile ilichoelezwa kuwa walishindwa kueleza endapo zoezi la kuwaondoa kwenye vijiji vyao lilifanyika ndani au nje ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Uamuzi wa kesi hiyo 27/2017 ulisomwa na Jaji wa mahakama hiyo, Justice Nyachaye ambaye alisema mahakama imetupa shauri hilo baada ya kukosa sifa za kuwa mahakamani hapo hivyo kuzitaka pande zote kubeba gharama zao.
Shauri hilo linalovuta hisia za wengi lilifunguliwa mahakamani hapo septemba 12,2017 na wananchi wa vijiji vya Olososokwani, Olorien, Kirtalo na Arashi.
Mshitakiwa akiwa ni Mwanasheria mkuu wa serikali ambapo waleta maombi hao walieleza vijiji hivyo vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria kwenye wilaya ya ngorongoro
Waleta maombi walidai kuwa walitakiwa kuondoka kwenye vijiji hivyo kwa ajili ya uhifadhi wakati ardhi hiyo ni yao ya asili na walikuwa wakiitumia
Jaji Nyachae akisoma ushahidi wa waleta maombi alimtaja shahidi mmoja aliyeeleza kuwa alishuhudi polisi walifika kijijini kwao na kuchoma maboma moto akasema alipata hasara ya fedha na kondoo143 na mifugo wa majirani waliibiwa.
Mwisho