Site icon A24TV News

TCU MWAKA WA FEDHA 2022/2023 YATENGA BILIONI 6.4 KUIMARISHA UTHIBITI UBORA.

Na Doreen Aloyce, Dodoma.

IMEELEZWA kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 6.4 kupitia Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi kwaajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu ambapo zaidi ya mitaala 300 ya vyuo vikuu iko katika hatua mbalimbali zakufanyiwa mapitio.

Akizungumza Jijini Dodoma Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania TCU Prof.Charles Kihampa alipokuwa akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Time ya Vyuo Vikuu Tanzania kwa kipindi Cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya awamu ya 6 amesema lengo nikuhakikisha elimu itolewayo na vyuo vikuu Tanzania vinakidhi kiwango cha ubora kitaifa ,kikanda na kimataifa.

“Kwa mfano kuanzia mwaka wa fedha wa 2022/23 Serikali imetenga kiasi Cha shilingi Bilioni 6.4 kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi(Higher Education for Economic Transformation-HEET)kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya Vyuo Vikuu ambapo zaidi mitaala 300 ya Vyuo Vikuu iko katika hatua mbalimbali za kufanyiwa mapitio ili kuhuishwa kwa kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali ili kukidhi matarajio yao na mahitaji ya soko,

Katika kufanikisha hili tume ya vyuo vikuu Tanzania imeendelea kuandaa na kuratibu mafunzo ya kubadilishana uzoefu kwa viongozi na wanataaluma wa vyuo vikuu kuhusiana na uendeshaji wa Vyuo Vikuu utengenezaji mitaala inayozingatia ujuzi na inayoendana na soko,mbinu za ufundishaji kwa wahadhiri ambao hawakusoma fani za ualimu,ulinganifu wa programu za masomi(programme benchmarks),uthibiti ubora na utengenezaji na utumiaji wa mifumo ya komputa,”amesema.

Kadhalika Prof.Kihampa amesema Tanzania imeendelea kuwa Taifa la watu wenye maarifa ,ujuzi,weledi na uwezo wa kutatua changamoto za kijamii na uchumi kwa manufaa ya wananchi wake ifikapo mwaka 2025 pamoja na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na uwepo wa viwanda.

“Katika kuhakiki ubora TCU imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara wa kawaida na wa kushtukiza Kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa elimu itolewayo na vyuo vikuu hapa Nchini inakidhi viwango vya ubora kitaifa,kikanda na kimataifa,

Kwa mfano katika kipindi Cha julai 2021 hadi Februari 2023 vyuo vikuu vyote 47 vilivyopo vimekaguliwa na kupewa ushauri wa maeneo yanayohitaji kuboresha,”alisema.

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ni Taasisi ya Serikali, iliyoundwa mwaka 2005 kwa Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania. TCU ilitokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa lililokuwa Baraza la Ithibati la Elimu ya Juu (HEAC) lililoanzishwa mwaka 1995 kwa Sheria ya Elimu Sura ya 523 ya Sheria za Tanzania.

Mwisho.