Site icon A24TV News

WALANGUZI ACHENI KUWALAGHAI WAKULIMA

Na Doreen Aloyce, Dodoma

Kufuatia kuwepo kwa vitendo vya ulanguzi usio halali wa mazao kwa wakulima hapa nchini Bodi ya usimamizi wa Stakabadhi Za Ghala (WRRB) imetoa wito kwa walanguzi wa mazao kuacha kuwalagai wakulima kwa lengo la kujinufaisha.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Bodi hiyo Asangye Bangu Wakati akielezea utekelezaji wa bodi hiyo kwa waandishi wa habari ambapo amesema hali hiyo imeifanya Serikali kuchukua hatua ya kuanzisha mfumo ambao utasaidia kuondoa hali ya sintofahamu kwa wakulima.


Ambapo Bangu amesema kuwa kumekuwa na wimbi la watu wanakwenda mashambani kwa wakulima na kuwadalalia mazao na kununua kwa bei ya chini kitu ambacho kinaendelea kudidimiza maendeleo ya wakulima.

“Natoa wito kwa madalali waache kuwarubuni wakulima wawaache wajiunge katika Mfumo wa Stakabadhi ghalani ili waweze kuuza mazao yao kwa bei ya ushindani iliyopo sokoni kwa kuendelea kuuza mazao shambani inaendelea kuwadidimiza wakulima kwa sababu madalali wengi wananunua mazao kwa bei ya chini tofauti kabisa na bei iliyopo kwenye mfumo,”amesema Bangu

Bangu amesema mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghalamni pamoja na ongezeko la bei za mazao, mapato ya mkulima na mapato ya Serikali kwa wastani wa asilimia 200% kutokana na urasimishaji, ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 12% kwa mwaka,kichecheo cha ubora wa mazao yanayofikishwa sokoni

Ametaja mafanikio mengine ni upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayopita kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, ongezeko la mapato ya uhakika kwa Serikali Kuu na Serikali Mitaa na kukuza huduma za fedha vijijini,kufanikisha uanzishaji wa Soko la Bidhaa Tanzania.

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2020/21 ukuaji wa uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa 12% kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa 2% kwa mwaka kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Pia amesema Bodi imeweka mikakati ya kuanzisha maghala ya kisasa ya bei nafuu pamoja na kutoa elimu kwa jamii .

Bodi ya usimamizi wa stakabadhi za ghala ni Taasisi iliyopo chini ya wizara ya viwanda na Biashara iliyopewa majukumu ya kutoa leseni kwa waendesha ghala usajili na kuingiza taarifa za wadau muhimu wa mfumo iliyoundwa na sheria namba kumi ya mwaka 2005.

Mwisho.