Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa ufafanuzi kuhusu watahiniwa waliofutiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2022.
Akitoa ufafanuzi huo Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema kati ya watahiniwa 560,335 waliofanya mtihani, 337 ndio waliofutiwa matokeo na wengine 20 matokeo yao yamezuiliwa yakisubiri uchunguzi kukamilika.
Waziri Mkenda amesema kuwa kati ya waliofutiwa matokeo wanne waliandika lugha isiyo na staha, 51 walikutwa na maandishi yasiyoruhusiwa ndani ya chumba cha mtihani, 10 walikamatwa na simu na smart watch, 9 walifanyiwa mtihani na watu wengine na 27 walikamatwa wakisaidiana katika chumba cha mtihani.
“Wengine sita kutoka kituo cha Mnemonic, Zanzibar waligundulika kutumia jukwaa la WhatsApp kupata majibu kutokana na yule mmoja aliekutwa na simu, 206 walikuwa na mfanano wa majibu usio wa kawaida ukihusisha kituo cha mtihani cha Thaqaafa, Mwanza na Twibhoki Mara , huku 24 wa kituo cha Cornellius ambacho pia kilikuwa na watahiniwa kutoka shule ya Andrew Father Memorial waligundulika kupewa majibu kabla ya kuingia chumba cha mtihani,” amefafanua Prof. Mkenda.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali inafanya jitihada kumaliza kabisa tatizo la udanganyifu na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watumishi wa umma wote watakaobainika kuhusika na udanganyifu huo.
“Gharama za kuendesha mitihani ni kubwa sana; kufanya udanganyifu ni sawa na uhujumu uchumi hivyo watumishi wote watakaobainika kuhusika watafukuzwa kazi na kushtakiwa,” amesema Prof. Adolf Mkenda.
“Kubwa zaidi ni kuwa na maadili na uadilifu. Mtoto mdogo akifundishwa kuwa ili afanikiwe ni lazima aibe, hiyo ni kulibomoa taifa. Lazima tuwe makini na tusimame kidete kuhakikisha tunasimamia maadili katika elimu yetu,” ameongeza Waziri Mkenda.
Aidha Prof. Mkenda amewataka wazazi na walezi ambao wanahitaji taarifa zaidi wawasiliane na Baraza la Mitihani au hata Wizara ya Elimu ili kupata ufafanuzi.
Mkenda ameongeza kuwa uchunguzi unaendelea kupitia jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali huku akieleza baadhi ya watuhumiwa wako chini ya ulinzi.
Mwisho.