Site icon A24TV News

BILIONEA LAIZER ALIPEWA FEDHA ALALI KULINGANA NA THAMANI YA JIWE LAKE

Na John Mhala,Mirerani

Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Madini ya Tanzanite,Yusuph Money amesema kuwa serikali haikufanya makosa kwa uamuzi wake wa madini ya Tanzanite ambayo hayajasanifiwa{rafu} kuuzwa katika Mji wa Mirerani kwani ilizingatia vitu vingi vya msingi hadi kufikia hatua hiyo.

Money alisema hayo jana katika Mji wa Mirerani mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa hadhara uliokuwa ukihutubiwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi{CCM},Daniel Chongolo aliyefanya ziara katika Mji huo wenye historia kubwa nchini na kusema kuwa wanaolazimiasha Madini ya Tanzanite rafu yauzwe nje ya Mirerani hawana hoja za msingi kwani wanachukulia uamuzi huo kisiasa.

Alisema kwa sasa serikali imeruhusu madini ya Tanzanite yaliyosanifiwa ambayo yameongezewa thamani kuuzwa nje ya Mirerani hususani katika maeneo ya vivutio vya kitalii,hotel kubwa za kitalii na maeneo mengine maalumu na kusema kuwa hilo wao haliwatii shaka kwani ndio biashara yenyewe na serikali imelidhia kwa mpangilio maalumu lengo ni kila mmoja kulipa kodi stahiki.

Mwenyekiti huyo alisema kwa sasa serikali iko katika hatua za mwisho mwisho kukamilisha jengo la kufanyia biashara ya madini ya Tanzanite litakalojulikana kwa jina la ‘’Tanzanite City’’ lenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5 hivyo wafanyabiashara wote wa madini hayo tunapaswa kuiunga mkono serikali kwa jitihada hizo za kukuza biashara hiyo na Mji wa Mirerani kwa ujumla.

Akizungumzia jiwe la Tanzanite lililonunuliwa na serikali kutoka kwa Bilione Saninue Laizer ambalo baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo tofauti juu ya ukubwa wa jiwe hilo na thamani ya fedha aliyopewa,Money alisema kuwa thamani ya jiwe haliangaliwi kwa ukubwa bali linaangaliwa kwa ubora na rangi yake na sio vinginevyo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa jiwe la Tanzanite linaangaliwa katika vitu vingi ili liwe na thamani kubwa ikiwemo ubora wa jiwe unaokwenda sambamba na rangi yenye ubora wa hali ya juu unaokubalika katika soko la kimataifa na ndio thamani yake inakuwa kubwa na sio kuangalia ukubwa wa jiwe bila kuzingatia vitu hivyo vinavyohitajika sokoni.

‘’Serikali ilinunuwa jiwe la Tanzanite kwa Bilionea Laizer kwa thamani ya jiwe na sio ukubwa wa jiwe na fedha aliyoipata iliendana na ubora wake na sio ukubwa’’alisema Money

Naye Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara ,Christopher Ole Sendeka alisema uamuzi uliotolewa na serikali juu ya soko la madini liwe katika Mji wa Mirerani haukufanywa kwa kukurupuka bali ulizingatia mambo mengi ya msingi kwa maslahi ya Nchi na wanataka soko hilo liwe katika Jiji la Arusha wana yao ila muda ukifika ataweka hadharani kwani wana maslahi yao binafsi na sio ya Nchi.

Sendeke alisema na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaaamini wafanyabiashara wa Tanzanite na kusogezea huduma ya soko katika Mji wa Mirerani na alimwomba Rais kuwafikiria juu ya suala la zana za uchimbaji kupunguziwa kodi ama kuondoa kwani kwa sasa ziko katika gharama kubwa na upatikanaji wake ni wa shida.

Alisema na kuwataka wafanyabiashara wa Tanzanite kumuunga mkono Rais katika jitihada zake za kuhakikisha biashara hiyo inafanyika katika Mji wa Mirerani ikiwa ni pamoja na kulipa kodi stahiki na kuwapuuza wale wote wanaotaka biashara hiyo kufanyika katika Jiji la Arusha.

Mwisho