CHAMA cha Mapinduzi CCM kupitia jumuiya ya wazazi mkoani hapa, kimejitosa kupambana na ukatili wa kijinsia wilayani Arumeru huku kikipinga adhabu ya fimbo 70 kwa vijana wanaoenda kinyume na maadili.
Pamoja na hatua ya wazee wa ukoo (Washiri)wilayani humo kutumia mila zao kuwarekebisha vijana kwa kuwachapa fimbo 70 ,chama hicho kimesema ipo haja kutazamwa upya umuhimu wa kuendelea na mila hizo ,kwani zinachochea ukatili
Katibu wa jumuiya ya wazazi Mkoa wa Arusha Deogratias Nakey ameyasema hayo wilayani humo, alipokuwa akiongea na wanachama wa ccm wakati kamati ya utekelezaji ya umoja wa wazazi mkoa wa Arusha,ilipotembelea wilaya hiyo kukakugua uhai na maendeleo ya jumuiya hiyo pamoja na utoaji wa elimu masuala ya ukatili wa kijinsia.
Alisema kuwa matukio ya ukatili yamekuwa yakishamiri kila wakati kutokana na maadili kuporomoka miongoni mwa jamii,hivyo aliwataka wananchi kukemea kwa nguvu zote na kuwa mstari wa mbele kufichua.
“Nani ametuloga hadi tunasahau maadili yetu,watu wa Arumeru niwaombe tukemee kwa nguvu zote ili matukio ya ukatili yasijirudie ,tujenge urafiki na watoto wetu ili watusaidie kufichua maovu”
Awali mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Meru,Nangera Nanyaro alisema suala la kuchapa viboko 70 kwa vijana wasio na nidhamu ni utaratibu walioukuta kutoka kwa wazee wa Mila ila wataendelea kukemea adhabu hiyo .
“Nisiseme kwamba kuchapa ni ukatili ila ni utaratibu uliowekwa na wazee wetu wa mila na desturi kwa lengo la kufundisha na kuonya vijana walioharibika kitabia kwa unywaji wa pombe misibani na kwenye ibada “
Aliongeza kuwa wataendelea kutoa elimu ili kuzuia matukio ya utovu wa nidhamu yasitokee ili viboko 70 visitumike.
Naye katibu wa jumuiya hiyo wilaya ya Meru,Jane Mollel alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua uhai wa chama na kutoa elimu juu ya matukio ya ukatili katika kata mbalimbali wilayani humo.
“Jambo kubwa tunalohimiza kwa wazazi ni kuacha ukatili wa kijinsia hivyo kupitia jumuiya ya wazazi tumekuwa tukikemea na kutoa elimu ili watu wawe na utaratibu wa kutoa taarifa matukio ya ukatili”
MWisho .