Na Doreen Aloyce, Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt.Amos Nungu amewataka watanzania kuziamini na kuzitumia bunifu zinabuniwa na vijana wa kitanzania ikiwemo kuzinunua na kurejesha mrejesho kwa wabunifu kama sehemu ya kuziboresha.
Ametoa kauli hiyo leo Aprili 27,2023, wakati anazungumza na waandishi wa habari ,katika banda la Tume hiyo liliopo katika maonesho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania yanayoendelea katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
“Niwaombe watanzania tuwatie moyo wabunifu wetu wanaopambana kila kukicha kubuni vitu ambavyo vitasaidia kuondoa changamoto katika jamii na mkivitumia kama kuna upungufu au kasoro utabaini usiache kuwarejeshea maoni ya kurekebisha ili ubunifu huo uweze kutumika kwa manufaa ya watanzania na taifa kwa ujumla,”
Na kuongeza kuwa “Sisi COSTECH kwa mfano katika MAKISATU yaliyopita kuna kijana alibuni gari ya kutumia mfumo wa umeme lakini alivyokuja kwetu tukabaini mapungufu na tukamdhamini kwa kumpatia kiasi cha shilingi milioni 10 ili akaboreshe yale mapungufu,” amesema Dkt.Nungu.
Sambamba na hilo Dk.Nungu amesema kuwa kuna kila sababu ya vijana wa kitanzania kutambua na kuamini juu ya ubunifu unaofanywa nchini Tanzania badala ya kusifia bunifu za nje ya nchi.
“Kwa sasa serikali kupitia COSTECH imeweza kuwaweka sokoni vijana wengi ambao wameonekana kuwa wabunifu kwa kuwapatia vibali vya kuwaendeleza na kuwajengea uwezo wa kiuchuni jambo ambalo linaendelea kutoa hamasa katika jamii”,
Na kuongeza kuwa “Vijana wengi ambao wanajitokeza kwa kujitambulisha kuhusu ubunifu walionao wamekuwa wakisaidiwa kwa kuendelezwa au kuunganishwa katika mashirika mbalimbali ambayo yanakuwa yana uwezo wa kiutendaji kulingana na ubunifu alio uonyesha,”amesema Dkt.Nungu
Kuhusu wabunifu ambao wanabuni vifaa ambavyo ni hatarishi kama vile gobore au bunduki amesema kuwa wanatakiwa kuwasiliana na COSTECH kabla ya kuingia sokoni kwa kuuza bidhaa hizo.
Amesema kuwa serikali kazi yake kubwa ni kuwawezesha na kuwajengea uwezo wabunifu ambao wanaonekana kubuni vifaa hatarishi kwa kulinda usalama wa nchi na siyo kazi ya serikali kuwakamata na kuwaweka ndani.
Maonesho hayo yameandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kushirikisha ni Taasisi za Elimu ya Juu, Taasisi za Utafiti na Maendeleo, Vyuo vya Ufundi, Mashirika na Taasisi za Umma, Mashirika na Taasisi binafsi za teknolojia, Wizara mbalimbali na Wabunifu walioendeleza katika programu ya MAKISATU na kufikia hatua ya ubiasharishaji.
Lengo likiwa ni kuwakutanisha wabunifu mbalimbali ambapo wanatumia maonesho hayo kama jukwaa la kuonesha bidhaa zao mpya ambazo wamezibuni kupitia Taasisi zao ili jamii ione na kuvichukuwa kwa ajili ya kwenda kuvitumia kwa kutatua changamoto zao na kurahisisha utendaji katika shughuli za kila siku.