Site icon A24TV News

FAMILIA MOJA YAPOTEZA NDUGU WATANO, WAFARIKI DUNIA GARI YABEBWA NA MAJI ARUMERU MKOANI ARUSHA

Na Geofrey Stephen ,Arusha

Watu watano wa Familia moja wamefariki Dunia  baada ya gari yao aina ya Noah yenye namba za usajili 499 DMY kusombwa katika barabara ya Arusha-Moshi eneo la kata Amalula Tarafa ya King’oli Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,Emanuel Mtatifikolo aliwataja waliokufa na miili ya kuonekana ni pamoja na Angela Metili{26},Martha Metili{40} na Colin Lyimo{16} mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Ilboru Arusha.

Mtatifikolo alisema maiti mbili ambazo miili yao bado haijapatikana baada ya kupelekwa umbali mrefu na maji ni pamoja na mwili wa Brenda Amani{26} mfanyabiashara na mkazi wa Ilbolu na Lisa Metili{8} mwanafunzi wa shule ya Msingi Ilboru Arusha.

Alisema kuwa dereva wa Noah alitambuliwa kwa jina la Neiman Metili yeye alitoka akiwa mzima baada ya kufanikiwa kuchomoka katika usukani na kutelekeza gari lililosombwa na maji yaliyokuwa na kasi kubwa.

Mkuu wa Wilaya hiyo alitoa pole kwa familia,ndugu na jamaa waliopoteza wanafamilia kwani msiba walioupata ni msiba mkubwa sana kwani wanafamilia walikuwa wakienda katika mahafali ya kidatu cha sita Mkoani Kilimanjaro.

Alisema katika gari hiyo iliyokuwa na watu sita ni mtu mmoja tu Neiman Metili ambaye ni dereva aliokoka lakini amepoteza Mke wake Martha katika ajali hiyo.

Mkuu huyo alisema maiti zote zilizopatikana ziko katika hospital ya Nnkoaranga Arumeru zikisubiri taratibu za ndugu kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwa familia hizo katika eneo la Ilboru Arusha.

Mtatifikolo alitoa onyo kwa wakazi wa wilaya ya Arumeru kutodharau maji yanayopita barabara,mito na maeneo mengine kwani maji hayo huwa yana madhara makubwa kwa kuwa yanakuwa na kasi kubwa.

Alisema kuwa mvua kubwa inayonyesha katika Mkoa wa Arusha hususani katika wilaya ya Arumeru maji yake huvuka juu ya barabara ya Arusha –Moshi na maji hayo huwa yana kasi kubwa sana hivyo wenye vyombo vya usafiri wasiwe na haraka wasubiri hadi maji hayo yapungue.

Mkuu wa Wilaya alisema kuwa jeshi la zimamoto Mkoani Arusha linaendelea na jitihada za kusaka miili mingine amabyo haijapatikana katika ajali hiyo.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha,Kamishina Msaidizi,Justin Masejo hakuweza kupatikana kuelezea ajali hiyo kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa hadi tunakenda mtamboni.

Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo walisema kuwa maji yalikuwa mengi yakipita juu ya barabara ya Arusha-Moshi na baadhi ya magari yalisimama kusubiri maji kupungua lakini dereva wa Noah alikaidi na kulazimisha kupita na kumkuta yaliyomkuta.

Walisema vifo vya maji katika kipindi hiki huchangiwa na ukaidi wa madereva hivyo waliomba polisi kuwa macho kipindi mafuriko yanapotokea sehemu yoyote Arusha.

Mwisho