Site icon A24TV News

HABARI ZA HIVI PUNDE ! SABAYA AKIRI MAKOSA KULIPA FIDIA YA SHILINGI MILION 5 MAMA MZAZI AMWAGA MACHOZI NJE YA MAHAKAMA

Na Mwandishi wa A24Tv

Sabaya achiwa huru mama yake mzazi amwaga machozi nje ya mahakama ALIYEWAHI kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, leo April 5, 2023 ameachiliwa huru na mahakama baada ya kufutiwa mashtaka saba yaliyokuwa yakimkabili, ikiwemo uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka na kuongoza genge la uhalifu.

Mahakama imetoa uamuzi wa Lengai Ole Sabaya kulipa kiasi cha shilingi milioni 5 kama fidia kwa mwathirika na hapaswi kufanya kosa lolote la jinai kwa muda wa mwaka mmoja.

Sabaya ambaye mapema asubuhi ya leo alifika kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Moshi, kabla uamuzi wa kuachiwa haujatangazwa, kupitia Kifungu cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 91 kifungu cha 1A, kesi yake ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2022 ilifanyiwa marejeo kama upande wa mshtakiwa ulivyoomba.

Mawakili upande wa Jamhuri waliiomba mahakama kubadilisha mashtaka ya Lengai Ole Sabaya kutoka kuwa ya kesi ya Uhujumu Uchumi na kufungua kesi yenye Mashtaka ya Makosa ya Jinai baada ya Lengai Ole Sabaya kuomba kufanya mazungumzo nje ya mahakama na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ombi hilo la Sabaya lilikubaliwa na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Salome Mshasha baada ya Mawakili wa Lengai Ole Sabaya kuridhia na kufutwa kwa kesi yake namba 2 ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2022.

Baada ya kuridhia hilo, kesi mpya aliyofunguliwa Sabaya ni kesi kesi ya Jinai Namba 31/2023 ambayo ndani yake kulikuwa na mashtaka mawili mapya dhidi yake, kosa la kwanza likiwa ni kuchukua madaraka ambayo siyo yake.

Imeelezwa kuwa Lengai Ole Sabaya na wenzake, Januari 19, 2021 katika eneo la Masama Mbosho wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, bila kibali walivamia duka la Alex Evarest Swai na kuchukua mali na kuzizuia na kujipatia kaisi cha fedha shilingi milioni 50.

Kosa la pili ni kuzuia upatikanaji wa haki ambapo Januari 19, 2021 katika maeneo tofautitofauti katika Wilaya ya Hai na Tulia jijini Arusha na maeneo tofauti ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama za kumfanya Alex Swai kuwa ametenda kosa la kukwepa kodi.

Baada ya kusomewa mashtaka, Sabaya alikiri kufanya makosa yote hayo mawili mbele ya hakimu Salome Mshasha.

Mwisho