Site icon A24TV News

KUMBUKUMBU YA SOKOINE !VITENDO KUMUENZI TUACHE UFISADI TUJENGE NCHI KWA UMOJA

Na Geofrey Stephen Monduli ARUSHA

KUMBUKIZI ya miaka 39 ya Hayati Moringe Sokoine aliyefariki kwa ajali ya Gari mwaka 1984 imefanyika leo katika kanisa  Katoliki Parokia ya Emairete Kigango cha Engwikie Monduli Juu Wilayani Monduli huku viongozi wa dini wakikemea rushwa ,ufisadi na kuhimiza kuyaenzi mema ya Marehemu
Paroko wa kanisa hilo,padri,Arnold Baijukie alisema kuwa hayati Edward Sokoine alikuwa ninkiongozi aliyeacha alama aliyepinga  masuala ya rushwa ,wizi wa mali za umma ikiwemo uhujumu uchumi.
Akiongoza ibada ya kumbukizi ya kifo cha Sokoine,Paroko Baijukie, alisema lengo la  kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha  marehemu Sokoine kilichotokea Aprili 12,1984 ni alama aliyoiacha katika historia ya nchi ya Tanzania
Alisema mwaka 1978 alikutana na hayati Sokoine huko Mkoani Kagera kwenye msitu mkubwa wakiwa wanakimbia vita vya Kagera  wao wakiwa wadogo na wazazi wao na marehemu Sokoine aliwaambia wasiwe na wasiwasi kwani wapo salama maana wao walikuwa   wadogo  na ndio siku ambayo alikutana naye  .
Alisema alisikitika kusikia alipata ajali hivyo kila mwaka  watu mbalimbali wanapokusanyika kufanya kumbukuzi hawakosei bali wanafanya kumbukizi ya historia yake na wengine watamsemea mengi.
“Tunamkumbuka Sokoine kwasababu aliacha alama aliyoweka katika familia yake na Taifa kwa ujumla sababu alisimamia haki ikiwemo kupambana na wahujumu uchumi”
Alisema hayati Sokoine alikuwa mkali,tumwombee kwa mungu apumzike kwa amani na hapa Monduli alikuwa na mpango wa kujengwa shule ili kuinua elimu kwa jamii ya masai na wengine kwa ujumla.
Aliisihi jamii kujali wengine kuliko familia kwani alikuwa tajiri lakini alisaidia jamii mbalimbali bila ubaguzi pia alikuwa na ndoto ya kuanzisha parokia alitoa ekari 129 na aliacha hati miliki ya kimila.
“Tunaomba ndoto alizotuachia tuzimalize kwa kujenga shule kwaajili ya kuinua elimu kwa jamii za kifugaji na kutoa rai kwa wake wa marehemu kutokuwa  wanyonge kwani watu wapo kwaajili yao ikiwemo kujengwa bwawa kwaajili ya wafugaji kunyweshea mifugo yao lakini sasa hivi bwawa linajaa matope lakini pia alipenda kulinda mazingira “
Baada ya misa ya shukrani ya maisha ya kukumbuku ya marehemu,salam mbalimbali zilitolewa ambapo kiongozi wa Mila jamii ya kimasai,Laigwanani Meijo Ikirsongo alisema marehemu Sokoine alikuwa ni kiongozi shujaa,mwadilifu na mzalendo haswa katika kusimamia haki huku mbunge wa Jimbo la Monduli,Fredy Lowassa alisema jina la Monduli limejengwa na marehemu Sokoine na yeye anaongoza jimbo hilo ikiwemo kuendeleza heshima ya Jimbo hilo.
Alisema anakumbuka kabla ya Waziri Mkuu Edward Lowassa alipomaliza uwaziri mkuu ,mke wa marehemu Sokoine alifika nyumbani kwake Monduli na kumpa mkono baba yake Lowassa kwakurudi salama na marehemu Sokoine alisimamia uhujumu uchumi na waziri mkuu mstaafu  Lowassa alisimamia elimu.
“Kila mwanamonduli ajiongeze na Taifa linamkumbuka kwa alama alizoziacha na sisi tulio hai tujiulize tukifa tutaacha alama gani ili wengine wakumbuke “
Wakati huo huo,askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) Philemon Lengasi alimuomba Rais Samia Hassan Suluhu kuchukua hatua kwa wale wote waliotajwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwani pia hayati Sokoine alipinga masuala ya rushwa na uhujumu uchumi.
Ambapo Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Joshua Nassari alisema yote yaliyosemwa kuhusu bwawa la maji,uhifadhi wa mazingira,elimu yatafanyiwa kazi kwani maisha bila maji hakuna mifugo hivyo bwawa hilo wataalam wa wizara ya mifugo walishakuja na litafanyiwa kazi ili wafugaji waweze kunyeshwa mifugo yao na jamii ipate maji.
Shekhe Wilaya ya  Monduli,Ahmed Kisanda aliomba serikali iboreshe zaidi maktaba zote nchini ili watu mbalimbali wasome vitabu na kumbukumbu ya viongozi mbalimbali waliofanya mambo mengi katika nchi hii.
Awali Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhili Maganya alisema hayati Sokoine alitengeneza alama na kuacha alama na kwaniaba ya CCM itaendelea kuienzi familia aliyoacha ikiwemo michango iliyotukuka ya Hayati Sokoine
“Huwezi kutenganisha familia hii na chama cha Mapinduzi sababu Hayati Sokoine inamchango mkubwa sana kwa chama na serikali kwa ujumla.
Ibada ya misa hiyo imehidhuriwa na familia ya hayati Sokoine wakiwemo wenyeviti wa CCM Wilaya ya Arusha,Longido,Monduli,Arumeru na Meru,makatibu wa CCM wilaya, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini, viongozi wa serikali,waumini mbalimbali,majirani,ndugu jamaa na marafiki.
Mwisho.