Site icon A24TV News

Maaskofu na wachungaji watakiwa kuwa na msimamo  mmoja katika kupinga maswala ya ushoga .

Na Geofrey Stephen Arusha.

Maskofu pamoja na wachungaji wa makanisa mbalimbali yanayopinga ushoga wametakiwa kuwa na msimamo mmoja katika kupinga maswala hayo sambamba na kukataa mahusiano kabisa na makanisa yanayounga  mkono maswala ya ushoga.

Hayo yalisemwa jijini Arusha na Askofu wa kanisa la kilutheri Afrika ya Mashariki (KKAM) jimbo la Arusha Mashariki ,Dk Philemon Mollel wakati akizungumza katika ibada maalumu ya kuwasimika  kazini wachungaji na mashemasi.

Dk.Mollel alisema kuwa,ni lazima maaskofu na wachungaji wawe na msimamo  mmoja katika kukemea vitendo hivyo vya ndoa za jinsia moja ambazo  zinaungwa mkono na baadhi ya makanisa sambamba na kukataa mahusiano na makanisa  hayo ,kwani  ni laana kubwa na inaipeleka  nchi sehemu ngumu sana.

“Katika dhana hizi ambazo tunaishi kuna makanisa ambayo kuna wachungaji mashoga na waumini mashoga na huku tunapoelekea sasa hivi ni bapaya sana kwani kwa mtindo huu ukristo unaenda kukosa nguvu kabisa hivyo ni  jukumu  la kila  mmoja wetu kuhakikisha anasimama katika nafasi hii kukemea vikali  swala hilo”alisema .

Aidha alisema kuwa,hali kwa sasa hivi imekuwa mbaya na vijana wetu wanapotea wote ni jukumu la kila mmoja kuiombea nchi na mabadiliko yanayoendelea hivi sasa kwani kuna viashiria kwamba ukristo upo  mashakani kupotea na kila mmoja anatakiwa kutambua kuwa ushoga  hauna toba.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuwajibika katika makuzi  ya watoto  wao kwani wamekuwa bize na shughuli za maisha  na kuwaachia  jukumu  hilo  watu wengine wakiwemo wasichana wa kazi za ndani jambo ambalo aliwataka kuwa makini kwani dunia ya sasa hivi imebadilika  haitakiwi  kumwamini  mtu yoyote.

Naye Msaidizi wa Askofu wa kanisa hilo,Dk Philemon Mollel (Monaban) aliwataka  wazazi kuwa mstari wa mbele kuzungumza na watoto wao kwani vijana wengi wanaingia kwenye vitendo vya ushoga wakiwa na umri mdogo kutokana na tamaa mbalimbali za fedha .

Aidha alilitaka kanisa kuwa mstari wa mbele kukemea na kupinga ushoga huku wakimwomba Mungu  atunusuru na laana hiyo kwani tunapoelekea  ni pabaya  sana na vitendo vinavyoendelea  ni chukizo kubwa mbele za Mungu.

“Tunawaomba wachungaji mliosimikwa  kazini  leo mkaanze  na jambo hilo  kwenye makanisani  wala msiogope kuzungumzia  swala hilo  kwani hali  imekuwa mbaya sana na hatujui  tunapoelekea. “alisema .

Naye Mmoja wa wachungaji  waliosimikwa kazini ,Mchungaji Pendael Yohanes alisema kuwa, kanisa lina wajibu mkubwa wa kukemea swala la maadili kwani kwa sasa hivi maadili yameporomoka  sana na kanisa ndo lina nafasi kubwa ya kuzungumza na waumini wake kuhakikisha maadili  yanafuatwa.

Mwisho.