Site icon A24TV News

MFUMO BORA WAHITAJIKA KATIKA UOKOZI NA UTAFUTAJI MAENEO YA MAJI.

Na mwandishi A24tv .

Naibu katibu mkuu Uchukuzi Dkt. Alli Possi amewataka wadau wa sekta ya Majini na Anga katika eneo la utafutaji na uokoaji kuangalia namna wanaweza kuwa na mfumo bora watakaotumia katika shughuli zao.

Dkt. Possi ameyasema hayo leo April 24,2023 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wadau wa utafutaji na uokozi kutoka sekta za Anga na Majini .

Alisema serikali kwa sasa imefika katika kiwango kikubwa katika sekta ya Anga na Majini hivyo Uokoaji na Utafutaji ni jambo la muhimu ili kuhakikisha usalama wa vyombo na maeneo hususan majini yanakuwa salama.

” Wataalam lazima watambue nchi yetu na bara la Afrika linakabiliwa na changamoto gani na kuhakikisha wanakuja na masuluhisho yapi, nafahamu kama nchi zetu zinakosa vifaa vya kisasa vya utafutaji na uokoaji pamoja na tatizo la kibajeti na ishu ya mfumo gani utumike wataalam wakae na kutoa mapendekezo kwa saerikali ” Alisema Dkt. Alli Possi Naibu katibu mkuu Uchukuzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC ) Kaimu Abdi Mkeyenge alisema mafunzo hayo yataenda kuwawezesha wadau kuwa wazuri katika maeneo hayo pamoja na kuwaweka karibu na shirika la TASAC kwa ajili ya programu nyingi zinazoweza kuja nchini kama fursa za kukuza vipaji na uwezo wa wadau wanaohusika katika sekta ya Usafiri majini.

Mafunzo hayo ya siku tano yameandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC ) na Shirika la Bahari Duniani ( IMO ) yakitolewa na wakufunzi wa kimataifa yakiwa na lengo la kuwaandaa kuweza kukabiliana shughuli za utafutaji na uokoaji kwenye majanga au ajali zinazoweza kutokea katika maeneo ya maji.