Site icon A24TV News

Serikali kufunga Mkongo wa mawasiliano Wilaya 23 Nchini.

Na Doreen Aloyce, Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesaini Mkataba wa upanuzi wa mkongo wa Taifa na mawasiliano katika wilaya 23 unaogharimu takribani Bilioni 37.4.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kuwa Mradi huo unalenga kumaliza changamoto za mtandao katika wilaya hizo.

Amesema kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imepanga kutekeleza mradi wa kuimarisha mawasiliano katika ngazi ya Wilaya kwa kuunganisha Wilaya zote kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa mawasiliano ambayo yatachochea maendeleo katika Wilaya hizo, sambamba na wananchi kupata intaneti yenye kasi.

“Leo hii tunaenda kushuhudia utiaji wa saini Mkataba wa upanuzi wa Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL
na Kampuni ya HUAWEI International kwa ajili ya ujenzi wa Kilometa
1,520 ambazo zitaunganisha kwenda katika Wilaya 23,”amesema.

Waziri Nape amesema kuwa Kukamilika kwa mradi huo utaondoa changamoto za mawasiliano katika Wilaya 23 ambazo zitaunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

“Wilaya hizo zinaenda kuwa na mawasiliano ya uhakika na
yenye ubora ambayo yatasaidia katika shughuli za maendeleo na ujenzi wa
Taifa letu,

Malengo yetu kama Wizara kuhakikisha tunafikia lengo la kuunganisha Makao Makuu ya Mkoa na Wilaya ili kutoa fursa kwa serikali ya Mkoa na Wilaya kuimarisha mawasiliano ya ndani na pia kutoa fursa kwa Taasisi Umma na Binafsi kufikisha huduma zao kwa wananchi kwa haraka,”amesema Waziri Nape.

Kadhalika amesema kuwa Serikali kwa kutambua changamoto ya Wilaya zetu kukosa mawasiliano ya uhakika ambayo yamesababisha Wananchi katika Wilaya hizo kukosa fursa mbalimbali za kijamii na kibiashara hivyo imejipanga kuzitatua.

Ameeleza kuwa Mikoa yote nchi nzima imeishaunganishwa katika Mkongo wa Taifa na Mkongo umefika katika vituo vya mipakani ambavyo vimepakana na nchi jirani, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi muhimu katika Ukanda huu wa
Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi Ttcl Bi Zuhura Muro ameshukuru Serikali chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuwezesha utekelezaji wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenda kwenye ngazi ya Wilaya.

Hakika, Leo ni siku muhimu kwa Shirika letu na Taifa kwa ujumla kwa uwekezaji huu ambao unaenda kuimarisha sekta ya mawasiliano Nchini na kuchangia katika kukua kwa sekta nyingine za maendeleo,

Shirika la Mawasiliano Tanzania siku ya leo tunatia saini mkataba kati yetu TTCL na Kampuni ya HUAWEI International, mkataba huu ni wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenda katika Wilaya 23 ikihusisha ujenzi wa Kilometa 1,520,”amesema.

Aidha amesema Upanuzi huu wa Mkongo wa Taifa unakwenda sambamba na Dira na Malengo ya Shirika katika kuhakikisha inakuwa mtoa huduma bora wa miundombinu ya mawasiliano data na simu Kitaifa na Kimataifa,huku alisisitiza kuwa Bodi ya Wakurugenzi itashiriki kikamilifu katika kuhakikisha Menejimenti inasimamia vyema mradi huo na miradi mingine inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Awali akitoa taarifa ya Shirika hilo Mkurugenzi Mkuu Ttcl Mhandisi Peter Ulanga amesema mkataba huo ambao utasiniwa kati ya Ttcl na HUAWEI International Co. Limited unatakiwa kukamilika ndani ya miezi 6 tangu kusainiwa kwa mkataba huo.

“Kukamilika kwa mradi huu utaondoa changamoto iliyokuwepo awali ya ukosefu wa Mawasiliano katika wilaya 23 Kwa kuwa kuna wilaya zilikuwa hazina kabisa mawasiliano ya uhakika na nyingine zilitumia Teknolojia ya microwave Radio ambayo Teknolojia hiyo ilikuwa na changamoto ya kuathiliwa na hali ya hewa sambamba na changamoto za uwezo mdogo hivyo kushindwa kutoa huduma ipasavyo,”amesema.

Mwisho