Site icon A24TV News

WAZIRI MCHENGERWA TUMIENI MAWAKALA NA MABALOZI KUTANGAZA UTALII WA TANZANIA DUNIANI

Na Geofrey Stephen Stephen

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa waheshimiwa mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kushirikiana na makampuni ya mawakala ya utalii katika nchi husika kuwaleta watalii nchini ili kuifikia azma ya kuwaleta watalii milioni tano ifikapo 2025 na kukuza uchumi wa nchi.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Mei 18, 2023 wakati akisoma hotuba yake kwenye mkutano maalum wa kibiashara baina ya makampuni makubwa duniani ya watalii kutoka nchini China na wadau wa utalii nchini jijini Arusha alipokuwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Anderson Mutatembwa.

Amempongeza Balozi wa Tanzania nchini China kwa kushirikiana na wadau wengine kuratibu ujio wa mawakala hao na kutoa wito kwa mabalozi wengine kuiga mfano huo.

Amefafanua kuwanchi ya China ni soko la kimkakati la utalii kwa Tanzania kwa kuwa ni miongoni mwa nchi yenye watalii wengi ambao Tanzania inapaswa kunufaika nalo.

Akitolea mfano amesema kuwa nchi ya China inatoa takribani watalii milioni 155 kwa mwaka kwenda sehemu mbalimbali duniani lakini ni watalii 33000 kutoka china ndiyo wanaotembelea Tanzania kwa mwaka.

Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania na Ubalozi wa Tanzania nchini China wameandaa program maalum hii inayolenga kuwavutia watalii wengi kutoka China kuja kutembelea Tanzania.

Amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine program hiyo itahusisha masuala ya mafunzo ya utamaduni, masuala ya lugha, mifumo mbalimbali ya kurahisisha malipo wakiwa nchini, vyakula vya kichina na namna ya kujitangaza.

Aidha, amesema program hiyo itawasaidia watalii kutoka China kufurahia utalii wa Tanzania, pia kuratibu safari za kitalii ikiwa ni mwendelezo wa program ya Royal Tour iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Waziri Mchengerwa amesema mawakala hao ikiwa ni kundi lenye ushawishi mkubwa kwenye mnyororo wa thamani wa utalii duniani litasaidia pia kufungua milango ya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya utalii hapa nchini.

Amewapongeza wadau mbalimbali wa utalii nchini ambao wameshirikiana na Serikali katika kuratibu ujio huu wa mawakala hao huku akisisitiza kuwa kwa sasa Serikali itaongoza katika kufanya kushawishi badala ya kubaki nyuma kama na kuacha kazi hiyo kufanywa na wadau pekee.

Amesema Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo havipatikani katika sehemu nyingi duniani hivyo ina kila sababu ya kuweka mikakati mizuri ili kuwavutia watalii na wawekezaji ili waje nchini na kuleta fedha za kigeni.

“Ninaamini taifa letu ni taifa la kipekee, taifa ambalo lina vivutio vingi ambavyo mataifa mengi hayana na yanatamani kuwa katika nafasi kama yetu, pia vivutio vyetu ni vivutio ambavyo sehemu nyingi ya dunia havipo na ndiyo maana katika takwimu za UNESCO tunaongoza katika nafasi za juu kabisa. “amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Amewahakikishia mawakala hao kuwa tayari Serikali imeshaainisha maeneo ya uwekezaji katika hifadhi na kwamba imeandaa mazingira rafiki yatakayowezesha kufanya biashara na kupata faida.

Mara baada ya mkutano huu mawakala hao ambao wameambatana na vyombo vikubwa habari 6 kutoka nchini China wataembelea maeneo ya Hifadhi ili kuona vivutio vya utalii kabla ya kurejea nchini China mwishoni mwa mwezi Mei 2023.

Mwisho