Site icon A24TV News

(COSOTA) yatoa mafunzo kwa wabunge.

 

Na Doreen Aloyce, Dodoma

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepatiwa mafunzo kuhusu majukumu na fursa zilizopo katika ofisi ya Hakimiliki Nchini CoSOTA ikiwemo kulinda hakimiliki za Wabunifu hapa nchini.

Wakipatiwa semina hiyo katika ukumbi wa Msekwa bungeni jijini Dodoma na kufunguliwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ambapo amesema lengo ni kueleza fursa za kibiashara zilizopo katika Hakimiliki pamoja na kuongeza uelewa kuhusu taasisi hiyo.

“Sekta ya Ubunifu nchini inakua siku hadi siku, sisi upande wa Serikali tunandelea kuhakikisha Wabunifu wananufaika na kazi zao pamoja na kuwaelemisha kuhusu umuhimu wa kusajili kazi zao katika ofisi yetu ya COSOTA”, amesema Mhe. Chana.


Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa ofisi hiyo, Doreen Sinare amesema moja ya jukumu lake ni kuhakikisha Wasanii wananufaika na kazi zao ikiwemo kupata mirabaha kutokana na matumizi mbalimbali ya kazi hizo.

Aidha amefafanua kuwa mwaka jana Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki ambapo jukumu la kukusanya limeondoka na linakwenda kufanywa na Wabunifu wenyewe kupitia kampuni watakazozianzisha.

Nae, Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Prof. Kitila Mkumbo amesisitiza kuwa Serikali inakamilisha mchakato wa kusaini Itifaki ya Arusha kwani imechukua muda mrefu na jambo hilo ni la msingi kwani litasaidia kuitangaza nchi na kukuza ubunifu katika eneo la kilimo.

Kwa upande wa wadau wa uzalishaji wa maudhui ya Televisheni Azam Media na DSTV, waliwaomba Wabunge hao kusaidia kukemea vitendo vya wizi wa maudhui sababu kunapoteza mapato ya Serikali na kunadhoofisha uwekezaji uliyofanywa na makampuni hayo.