Na Geofrey Stephen Arusha
WAFANYABIASHARA wa kampuni ya Serengeti Holdings LTD ya jiji la Arusha,wametoa notisi ya siku 30 kwa halmashauri ya Jiji la Arusha kulipa kiasi cha sh, milioni 365 kutokana na hatua ya jiji hilo kuvunja mghahawa wao kinyume na utaratibu .
Aidha wafanyabiashara hao wanakusudia kuiburuza mahakamani halmashauri hiyo iwapo itashindwa kulipa kiasi hicho cha fedha baada ya kupokea notisi inayoanzia leo Mei 9 mwaka huu .
Akiongea na waandishi wa habari Wakili wa Wafanyabiashara hao,John Malya kupitia kampuni yake ya Uwakili ya Caden Dante Attorneys alisema kuwa wateja wake wamepata hasara na wanataka fidia ya shilingi milioni 365.
Alifafanua kuwa septemba 7, Mwaka 2007 Halmashauri hiyo iliingia makubaliano ya upangaji na wateja wake na mwaka 2011 wateja wake waliwekeza mradi wa mhagawa wa gari linalotembea katikati ya jiji la Arusha,wenye thamani ya sh,milioni 154 .
“Mteja wetu tangu mwaka 2011 aliwekeza kwa kuweka gari/trailer maalumu la kusimama sehemu moja (trailer lenye majiko ya kisasa ya gesi, mitungi ya gesi, jokofu, na freezer, vifaa vya kuzuia moto-fire sensor,) “alisema
Pia walijenga miundombinu ya kuwezesha kufanyika kwa biashara ya chakula ikiwa ni pamoja na jiko la kupikia pizza, banda la wateja/seating shade, (Benches) choo, matanki ya kuhifadhi maji, mtambo wa kuzalisha umeme wa jua (solar panel), jenereta la umeme, miundombinu ya kutoa maji taka na wa akiba umeme.
Wakili Malya alisema kuwa Mei 3 mwaka huu Halmashauri hiyo kupitia askari wake wa akiba walivamia eneo hilo na kufanya uharibifu kwa kuvunja miundo mbinu yote kwa madai kwamba ulijengwa kinyume na utaratibu wa mipango miji ya jiji hilo.
Kwa mujibu wa Malya anadai kwamba kuna mpango mchafu wa kibiashara wenye harufu ya rushwa na aliwatuhumu madiwani wa jiji hilo kuhongwa ili kumwondosha katika eneo hilo.
“Juzi nilisoma kwenye mtandao madiwani wa Arusha wanatuhumiwa kupokea rushwa ili kuruhusu mghahawa huo kuondolewa na kama hawajachukua jiji wajitokeza kukanusha ,nimetuma nakala Takukuru ili wachunguze jambo hilo”
Alidai kuwa mteja wangu alikuwa akiuza wastani wa shilingi 1.6 kwa siku na alitoa ajira kwa watanzania 15 na alikuwa akilipa mapato ya serikali bila usumbufu wowote ,hivyo kutoka na uharibifu huo anaitaka halmashauri hiyo kupitia Kaimu Mkurugenzi kumlipa kiasi cha shilingi milioni 365 kama fidia ya mali zilizoharibiwa na hasara ya kibiashara.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Hargeney Chitukuro, alisema kuwa uamuzi wa ubomoaji wa Mgahawa huo uliamuliwa na Kamati ya Mipango Mji iliyochini ya Uenyekiti wa diwani wa Kata ya Lemara aliyemtaja kwa jina la Nabort Silasi na sio uamuzi wa Mkurugenzi.
Chitukuro alisema Wafanyabiashara hao waliombwa bila mafanikio kuwasilisha nyaraka mbalimbali za uhalali wa uwepo katika eneo hilo lakini hawakufanya hivyo na kusema kuwa eneo hilo si salama kwa biashara baada ya kuonekana kuna biashara ya kituo cha mafuta na Benki.
“Alipewa kibali cha mghahawa wa kutembea lakini yeye aliamua kufanya ujenzi wa kudumu katika eneo hilo na alipoombwa kibali hakutii amri hiyo ndio uamuzi wa kuvunja mgahawa ulipoamuliwa “
Ends..