Na Richard Mrusha
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema imekuwa ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua migogoro baina ya maeneo ya Hifadhi na Wananchi huku ikisisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaovamia maeneo ya Hifadhi.
Hayo yamesemwa leo Mei 25 2023 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Momba, Mhe.Condester Sichalwe aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kutatua migogoro kati ya wananchi na maeneo ya Hifadhi za Taifa.
Amefafanua kuwa moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kutatua migogoro hiyo ni kufanya tathmini ya aina, chimbuko na namna ya kutatua mgogoro husika.
Amewaomba wananchi kujitahidi kuheshimu vyombo vya dola vilivyopo kwani viko kisheria na vinatekeleza majukumu ya kulinda rasilimali za nchi.
“Heshimuni vyombo vya dola kwani mnapowashambulia askari uhifadhi mnawapunguzia nguvu ya kulinda rasilimali za Taifa zilizoko hapa nchini” amesisitiza,Mhe Masanja.
Akizungumzia kuhusu Hifadhi zilizoko katika Wilaya ya Momba, Mhe. Masanja amesema hakuna mgogoro kati ya wananchi na misitu iliyoko Wilayani humo huku akitaja misitu hiyo kuwa ni pamoja na Msitu wa Isalalolunga, Isalalo, Ivuna north na Ivuna South.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na uharibifu katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuweka alama za kudumu za mipaka, kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii, kuondoa wavamizi na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wahalifu.