Site icon A24TV News

SERIKALI YAWEKA MIPANGO KABAMBE KUSHUKA KWA ALZETI NA MAFUTA NCHINI. Yakutana na wazalishaji

Na Doreen Aloyce,Dodoma

SERIKALI imekutana na wadau wa kuzalisha mafuta ya kupikia kwa ajili ya kujadili changamoto zinazosababisha kushuka kwa bei ya mafuta na alizeti nchini.

Kikao hicho kilicho kimefanyika leo tarehe  23 Mei, 2023 kilichowakutanisha mawaziri watatu kutoka wizara tatu ,waziri wa Uwekezaji, Viwanda , Biashara Mhe. Dkt Ashatu Kijaji , Waziri wa Kilimo Husssein Bashe na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba.

Akifungua kikao   hicho Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema lengo la kikao hicho ni kuongea kwa pamoja , kuboresha maisha kuchangia uchumi wa Taifa na hatimaye kuzalisha mafuta ambayo yatajitosheleza na hivyo kuachana na  kutumia fedha za kigeni kuagiza mafuta nje ya nchi.

Amesema kuwa kwa sasa Alizeti  imeshuka kwa asilimia 50 na   mafuta ya kupikia kwa asilimia 17 jambo ambalo limepelekea wananchi hususani wakulima kuwa na malalamiko hivyo serikali ikaona wajadiliane na kwenda pamoja .

“Tuna viwanda 771 vinavyochakata mafuta , tunazalisha tani laki tatu na mahitaji yetu ni tani laki tano na sitini hivyo mafuta bado hayatoshi hali inayopelekea kuruhusu wenzetu welete kutoka nje ya nchi na kupitia hali hiyo Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akaelekeza tuwe na Mikoa mitatu ya kilimo cha Alizeti ndani ya Taifa letu ambayo ni Dodoma, Singida na Simiyu lengo ni kutafuta malighafi ya kutosha”amesema Dkt Kijaji.

Pia amesema kuwa nguvu imewekwa kwa wakulima  na wameweza kuzalisha Alizeti ya kutosha na lengo ilikuwa kufikia uchumi shirikishi na kwamba kupitia kikao hicho wataondoa changamoto ili kukuza uchumi wa pamoja.

Nae  wa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba amesema kuwa ili kuondokana na changamoto hiyo kuna haja ya kutengeneza sera ya kuwakuza kiuchumi na kwamba ndani ya miaka mitatu serikali haitaagiza mafuta nje ya nchi.

Amewataka  wazalishaji wa mafuta ya Alizeti kuwaripoti maofisa wa Serikali wanaowataka kutoa Rushwa ili waweze kuchukuliwa hatua.

“Natamani tufanye vizuri sisi wazalishaji tuondoke kwenye umimi bali wote tuangalie tunapata nini kwenye huu mnyonyoro wa dhamani na hivyo viwanda vilivyofungwa inasikitisha sana wengine ni vitisho vya hao maofisa wa Serikali ambao mnashindwa kuwaripoti ” amesema Dkt. Mwigulu.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein  Bashe amesema kuwa wazalishaji wa mafuta wanapaswa kukutana wao kukaa kwa pamoja kuchagua uongozi mzuri ambao utawasaidia kuwaunganisha na serikali.

“Ninachotaka kuwaambia hapa mbele ya waziri ni kwamba wachakataji wa mafuta ya Alizeti waazishe taasisi ambayo itakuwa na umahili na sio chama cha  uanaharakati kwani imekuwa chanzo cha serikali kutokuwa kitu kimoja” amesema Waziri Bashe.

Nao washiriki wa kikao hicho wamesema kuwa kupitia kikao hicho wanategemea mapinduzi makubwa ili waweze kufanya uzalishaji ulio bora.

Aidha washiriki hao  akiwemo Nelson Mwakabuta Meneja wa Kampuni ya Mount meru Millas na Fatuma Salum mzalishaji  wamesema kuwa wamefurahishwa na kikao hicho na wana uhakika changamoto zilizowakabili ikiwemo upungufu wa malighafi na masoko yanaenda kupatiwa ufumbuzi.

“Tunaona taswira njema kupitia kikao hiki kwani tutapata mbegu ya uhakika , kiwanda kufanya kwa muda mrefu bila kutegemea msimu ” amesema  Nelson Mwakabuta.

Hata hivyo kikao hicho kimeleta tija kwa wazalishaji wa mafuta kutokana na majibu na mikakati iliyotolewa na Serikali huku wakiomba ushirikiano pande zote mbili jambo ambalo litasaidia kuinua uchumi wa nchi.

mwisho