Site icon A24TV News

BANK YA NCBA YAMWAGA VIFAA VYA TIBA KWA KITUO CHA AFYA KITUMBEINE

John Walter -Arusha.

Benki ya NCBA imetoa msaada wa vifaa tiba katika kituo cha Afya cha Kitumbeine kilichopo Wilayani Longido Mkoani Arusha kwa lengo la kuwasaidia wakinamama wajawazito wasioweza kujifungua kwa njia ya kawaida kufanyiwa upasuaji ili kuokoa Maisha ya Mama na Mtoto ambao walikua wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za upasuaji katika hospitali ya Wilaya.

Akikabidhi Msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NCBA Claver  Serumaga amesema kuwa benki hiyo imejizatiti katika kusaidia jamii inayowazunguka  na katika kipindi wameamua  kutoa msaada huo katika katika kituo cha Afya cha Kitumbeine kinachohudumia Zaidi ya watu 40,000.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa wametoa vifaa vya kufanya upasuaji kusaidia huduma ya upasuaji katika kituo hicho cha Afya  ambacho kitaanza kutoa huduma hizo hivi karibuni kwani watu wengi wanahitaji huduma hiyo.

“Msaada huu utasaidia kusogeza huduma za afya karibu na watu tumefurahi na tutaendelea kutoa misaada kwani huu ni mwanzo na tutaendelea kufanya kazi Pamoja”

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dr.Silvia Mamkwe akipokea msaada huo ameipongeza benki ya NCBA kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii ya watu wa Longido ambao ni wafugaji ili waweze kujifungulia katika vituo vya afya kwani tayari serikali imeboresha huduma za afya na kupeleka wataalamu wa afya wa kutosha.

Naye Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Longido  Dr.Selemani Mtenjela amesema wamepokea kitanda maalumu kwa ajili ya kupima mgonjwa Pamoja na vifaa vya kufanya upasuaji ambavyo vitasaidia kuokoa Maisha ya Wajawazito ambao walikua wakitembea kilomita 60 kufuata huduma za upasuaji katika hospitali ya Wilaya.

Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Kitumbeine Dr.Frank Albert  amesema kuwa kwa msaada walioupata watapunguza kutoa rufaa kwa wajawazito Kwenda hospitali ya wilaya kwani kwasasa wamejitosheleza kuanza kufanya upasuaji.