Site icon A24TV News

MBUNGE WA VITI MAALUM MKOA WA MANYARA AWATAKA WAZAZI KUPAMBANA NA UKATILI KWA WATOTO

Na John Walter-Manyara
Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Manyara Yustina Rahhi amewakumbusha wanawake na wanaume kujiweka karibu na malezi ya watoto ili Kupambana na Ukatiili kwa watoto kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti maeneo mbalimbali nchini.

Rahhi ameyasema hayo wakati akiwa kata ya Endamilay kwenye ziara ya kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya Wanawake wa chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Mbulu, katika yenye lengo la kuimarisha chama cha hicho na jumuiya hiyo pamoja na kutoa elimu kwa jamii katika mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia na watoto.
Rahhi amesema iwapo Wadau wote wataungana na Serikali itakuwa rahisi kupambana na vita dhidi ya ukatili wa kijinsia na watoto unaoendelea.

Amesema Wanawake wakiwa mstari wa Mbele kupambana na kuzuia vitendo vya Ukatili wa kijinsia hata wanaume wanaojihusisha na vitendo hivyo wataogopa na kuacha kabisa.

Aidha ameitaka jamii iendelee kuunga mkono jitihada za serikali katika kupinga vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na Ukeketaji kwa Wasichana na wanawake, ubakaji na ulawiti kwa watoto.

Mheshimiwa Rahhi amewataka wananchi kukemea vitendo hivyo kwa nguvu zote na kuwafichua wote wanaohusika bila kujali ni ndugu au kiongozi.
“Msikubali kuongwa pesa au chochote ili kumaliza kesi kimila kwa kuwa inachochea zaidi vitendo hivyo kushamiri katika maeneo mengi huku waathiriwa wakiendelea kuteseka” alisisitiza Rahhi.

Katibu wa UWT wilaya ya Mbulu Vijijini Pili John amesema ni wakati wa Wazazi na walezi kuwalea watoto kwa nguvu zote kuepuka tabia ya baadhi ya wazazi kumhudumia zaidi mtoto wa kike na kumsahau wa kiume na badala yake wawalee kwa usawa.

Mwenyekiti UWT Wilaya ya Mbulu Vijijini Yasinta Salaho amessema ni wakati wa jamii kuachana na tabia ya kusuluhisha kesi za ukatili kinyumbani ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Akiwa katika kijiji hicho cha Endamilay Mheshimiwa Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Manyara Yustina Rahhi, alipokelewa kwa shangwe na nyimbo mbalimbali na wananchi huku akiwasisitiza kuendelea kumuunga mkono rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulinda na kuitunza amani iliyopo nchini.

Mwisho .