Site icon A24TV News

MIRADI ,17 YENYE THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 2 KUZINDULIWA NA MBIO ZA MWENGE WA UHURU WILAYANI LUSHOTO

Na Geofrey Stephen Lushoto

Miradi 17 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2 inatarajiwa kuzinduliwa na Mbio za Mwenge Kitaifa katika wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga na Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili katika wilaya hiyo kesho na utazunguka katika Wilaya hiyo kwa umbali wa km 304.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Leo ofisini kwake,Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,Kalisti Lazaro alisema kuwa Mwenge utapokelewa Lushoto katika Kijiji Cha Samata kilichopo Halmashauri ya Bumbuli na utazungushwa katika Halmashauri hiyo kwa umbali wa km 122 na miradi 9 itazinduliwa yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 779.

Kalisti Lazaro akizungumza na Vyombo vya Habari ofisini kwakwe 

Lazaro alisema kuwa miradi itakayozinduliwa na kufunguliwa katika Halmashauri ya Bumbuli ni pamoja na miradi ya Afya,elimu,maji na barabara na miradi yote imekidhi viwango na imezingatia thamani ya pesa kwa mujibu wa Sheria ya manunuzi.

Mkuu huyo alisema kuwa Juni 14 mwaka huu Mwenge utapokelewa katika Halmashauri ya Lushoto katika shule ya Msingi ya Kizara na utakimbizwa umbali wa km 173 katika miradi 8 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.2

Alisema miradi itakayozinduliwa katika Halmashauri ya Lushoto ni pamoja na miradi ya Afya, elimu, maji na barabara yenye thamani ya kiasi hicho Cha pesa na miradi hiyo imekidhi viwango na vigezo hususani thamani ya Shilingi na kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma Kama ilivyowekwa na Serikali.

Lazaro amewataka wànanchi wote wa Wilaya ya Lushoto na viunga vyake kujitokeza kwa wingi pindi Mwenge wa Uhuru utakapopita barabarani na utakapo kwenda kuzindua miradi ya Maendeleo katika maeneo tajwa katika wilayani hiyo.

Mwisho.