Site icon A24TV News

PROFESA NDALICHAKO AFUNGUA MAFUNZO YA MAOFISA KAZI KUTOKA MIKOA 26 NCHINI TUJITUME KATIKA KAZI

Na Gofrey Stephen Arusha .

Prof Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ameonya baadhi ya maofisa kazi nchini wanaotumia lugha za vitisho kwa waajiri na kutumia vibaya majina ya viongozi pindi wanapoenda kufanya kaguzi sehemu za kazi.

Akizungumza jijini Arusha Waziri huyo akifungua mafunzo ya maofisa kazi kutoka mikoa yote 26 hapa nchini, yaliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya Ukimwi (UNAIDS), yenye lengo la kutoa mafunzo  ya ukaguzi sehemu za kazi kuhusu virusi vya Ukimwi na usalama kazini

Amesema kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa watakaobainika kutumia lugha za vitisho kwa waajiri na kutumia vibaya majina ya viongozi na kudanganya wamewatuma, watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Wengine wanaenda kwa waajiri wanatumia lugha za vitisho halafu wanasema nimetumwa na Waziri, Kamishna wa kazi au Katibu Mkuu, sheria zipo kwanini mtumie vitisho? Amehoji waziri huyo na kuongeza.

Kuhusu maadili amesema baadhi ya maafisa wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa wanapoenda kufanya kaguzi na kuwa wizara yake itawashughulikia watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo vimesabababisha kuleta taswira mbaya kwa serikali.

“Tuangalie suala la uadilifu tusipoteze imani kwa waajiriwa. Wanasema samaki mmoja akioza ni wote wameoza ila tumekubaliane samaki mmoja akioza tunamtupa ili wengine wabaki kuwa salama,” amesema.

Mratibu wa Ukimwi, usalama na afya mahali pa kazi kutoka ILO, Getrude Simon, amesema mafunzo hayo ya siku tano yameshirikisha maofisa wa kazi kutoka mikoa yote nchini na baada ya mafunzo wataenda kufanya kaguzi katika baadhi ya maeneo ya kazi na kuainisha masuala yanayohusu ubaguzi wa wafanyakazi wanaoishi na virusi vya Ukimwi na masuala ya kijinsia.

Amesema maofisa hao watawezeshwa namna bora ya kutumia mikataba ya kimataifa katika shughuli nzima za kufanya kaguzi pamoja na mkataba unaosimamia shughuli za kaguzi sehemu za kazi.

“Maafisa kazi hawa wana nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa waajiri namna ya kuwezesha watumishi wanaoishi na Ukimwi kufanya kazi bila ubaguzi na hii ni sambamba na mkataba wa Shirika la Kazi namba 111 unaohusu kuzuia ubaguzi sehemu za kazi ambao umeendelea katika baadhi ya maeneo ya kazi,”amesema.

Mwisho