Site icon A24TV News

ARUSHA WAZINDUA MTANDAO WA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA KWA JAMII ZA PEMBEZONI

Na Geofrey Stephen,ARUSHA

MKOA wa Arusha umezindua mtandao wa kupambana na ukatili wa kijinsia kwa jamii za pembezoni, ili kuongeza nguvu na kuwa na sauti ya pamoja ya kupinga na kutokomeza matukio hayo ambayo yanakithiri katika mikoa ya Arusha na Manyara.

Aidha wamesoma tamko la kutaka mabadiliko ya sheria ya ndoa na umri mdogo wa msichana kuolewa.

Akizungumza jana jijini Arusha wakati wa kufunga warsha ya siku mbili iliyoambatana na uzinduzi wa mtandao huo unaojumuisha mashirika kumi,Mkurugenzi wa Shirika la Mimutie Women Organization, Rose Njilo amesema mtandao huo utaratibiwa na shirika hilo.

“Sisi kwa miaka kumi tunapambana na matukio ya ukatili wa kijinsia hivyo tumeona ipo haja ya kuunganisha nguvu ili tuwe na sauti ya pamoja katika vita hii ili tupunguze matukio haya au kuyatokomeza kabisa hasa kwenye jamii za pembezoni ambazo haziwezi kufikiwa.

“Ukatili unaoongoza ni wa ndoa za utotoni na za lazima na vipigo kwa watoto hao na wanawake,kwenye mikoa ya Arusha na Manyara,”alisema.

Aidha, alisema wamefikia hatua ya kuzinduq mrandao huo, baada ya kuona matukio yanazidi kushamiri mikoa ya Arusha na Manyara,ambapo kwa mwaka 2022 walipokea kesi za ukatili wa kijinsia kwenye suala la ndoa za utotoni 14 ambazo nyingi ni za Arusha na chache Mkoa wa Manyara..

“Katika mwaka huu 2022 kesi moja tulishinda ya mtoto mmoja aliyeolewa katika umri mdogo na kupigwa ambapo Desemba 27 mahakama iliwatia wahusika hatiani na sisi wanaharakati tukapata ushindi,”alisema

Pia shirika lake limeokoa watoto 34 katika ndoa za utotoni na kuwapeleka shuleni na baadhi wanaendelea na masomo na wengine wanafanya kazi baada ya kumaliza kusoma.

Hata hivyo alisema pamoja na jitihada wanazofanya za kupinga ukatili wa aina mbalimbali kwa jamii za pembezoni bado jamii na baadhi ya wazazi wengi hawatoi ushirikiano kwao pale kesi zinapokwenda mahakamani na kusababisha kesi nyingi kukosa ushahidi.

Kadhalika, alisema mashirika yaliyojiunga kumi ni mwanzo na wanakaribisha wengine watakaopenda kuungana kupinga ukatili kwa watoto wao.

Kuhusu tamko lao, Rose alisema takribani miaka minne sasa serikali kupitia muhimili wa Bunge na Wizara ya Sheria na Katiba imeshindwa kutekeleza kwa wakati na kuchukua hatua stahiki za haraka kufanya marekebisho ya sheria ya ndoa mwaka 1971 vifungu vya namba 13 na 17 vinavyohusu umri wa kuolewa nankuoa kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Rufani .

“Hivyo tunaitaka serikali kujielekeza kwenye kutekeleza hukumu ya mahakama ya Rufani kuhusu umri wa kuolewa na kuwasilisha muswada wa mabadiliko ya sheria ya ndoa na kuweka umri wa miaka 18 kuwa umri wa chini wa kuolewa na kuoa kwa wasichana na wavulana na si vinginevyo,”alisema.

Pia alisema mtandao huo unataka serikali kupitia Wizara ya Katiba na sheria kuwasilisha sasa na kuhakikisha ushiriki wa wadau katika kutoa maoni kwenye muswada husika unazingatiwa ili kuwa na sheria inayozingatia jinsia na hatakua na vifungu vinavyoendeleza ndoa za utotoni nchini na kubariki ukatili kwa watoto.

Alisema suala hilo linahitaji sauti za makundi yote wapenda haki na usawa ustawi wa mtoto wa kike na kuwataka wabunge kufahamu wajibu wao wa kubadilisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 nankuweka umri wa miaka 18 ili kuwalinda watoto dhidi ya ndoa za utotoni bila kujali wapo shule au nje ya shule, sababu bado ni watoto na wanatakiwa kuwekewa mifumo ya kuwalinda na kuwekeza kwenye ustawi wao.

“Hakuna maendeleo tutakayofikia kama nchi bila kutokomeza ndoa za utotoni.Ndoa za utotoni zinaathiri wasichana wengi wa tabaka la chini ambalo ni maskini kuwa na sheria inayohamasisha ndoa hizo ni kuendeleza mzunguko wa umaskini katika Taifa na kuwanyima wasichana hasa wanaotoka familia maskini au vijijini haki yao ya msingi ya kulindwa utu wao na kufurahia utoto wao,”alisema.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha, Blandina Nkini akifunga warsha hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alipongeza mashirika hayo kwa kuunda mtandao huo na kuwaasa kuelekeza nguvu kubwa kwenye suala la malezi na makuzi katika jamii, kwa kuwapa kipaumbele mtoto wa kike na kiume katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Arusha, Flora Zelothe alisema mtandao huo anaamini utaleta mabadiliko chanya katika jamii, kwani kwa sasa wameelekeza kutetea watoto wa jinsia zote kike na kiume, tofauti na siku za nyuma, nguvu kubwa ilikuwa kwa mtoto wa kike.

1.Foma foundation
2.Embuan Devolvement organization
3.Elong foundation
4.Angonet
5.Dunia Salama Foundation
6.Maipak
7.Oseremi
8.Mimutie
9.Empath Foundation

Mwisho .