Site icon A24TV News

CHEMBA YA MKOSHA SENYAMULE KWA KUPATA HATI SAFI, ATOA ANGALIZO KWA WATENDAJI

Na Dorin Aloyce

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kwa kupata hati safi katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichojadili taarifa ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Pongezi hizo amezitoa katika kikao kazi cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo Wilayani Chemba.


“Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilikuwa na hoja 50 ambazo ambazo zimegawanyika katika sehemu tatu, hoja za mwaka jana 25, hoja za miaka iliyopita 25 na agizo la LAAC ambalo ni moja” ameeleza Mhe.Senyamule

Aidha, amesema kati ya hoja 50, 13 zimefungwa na 37 bado zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji chini ya Menejimenti ya Halmashauri na usimamizi wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.

Mhe. Senyamule amewaasa kufanya kazi kwa bidii, kuondoa tofauti baina yao na kutafuta namna nzuri ya usuluhishi wa tofauti zao zilizopo baina yao ili kuleta tija katika kuwatumikia wananchi.

‘’Chemba ni miongoni mwa Halmashauri ambazo taarifa za septemba 2022 zinaonyesha kuwa na tofauti katika taarifa zenu hivyo jitahidini kutafuta namna inayofaa kupata usuluhishi ili ziweze kuendana na kupunguza hoja za ukaguzi kila mwaka” Senyamule amesisitiza.


Mhe. Senyamule pia amesisitiza kamati ya fedha inayokutana kila mwezi kuwa na agenda ya kudumu ya kujadili mwenendo wa ujibuji wa hoja za ukaguzi za Mkaguzi wa ndani ili Halmashauri iweze kuondokana na changamoto ya kuwa na hoja nyingi zisizofanyiwa kazi .

Vile vile ameagiza Halmashauri hiyo kuweka mikakati ya kuhakikisha mapato yanaongezeka kufikia bilioni 2 kwa mwana na kufanya ubunifu mbalimbali wa vyanzo vya mapato.

Aidha amewataka kuhakikisha wanakamilisha Miradi ya maendeleo kwa wakati na ubora unaotakiwa ili kuendana na kasi ya viongozi wanatoa pesa ikiwa ni pamoja na miradi ya fedha za SEQUIP.

Kwa Upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Ally Gugu amewaasa Watumishi kuendeleza kushirikiana na Menejimenti vizuri ili kurahisisha utendaji na kuzingatia Sheria, taratibu, kanuni za utumishi wa umma bila kupoteza muda katika utendaji kazi .

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chemba Mhe. Sambala Said amesema kwa mwaka huu wa fedha Halmashauri hiyo imejipanga kivingine kila sekta kuonyesha utofauti na miaka mingine kama ilivyo fahamika kadhalika ameahidi ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya serikali.

Mwisho.