Site icon A24TV News

HISTORIA WAZIRI NAPE AZINDUA PROGRAM MPYA CHUO CHA UHASIBU NI YA KWANZA TANZANIA

Na Geofrey Stephen Arusha .
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye amezindua programu ya Shahada ya Media Anuwai na Mawasiliano kwa Umma katika chuo cha uhasibu Arusha-Kampasi ya Arusha .
Akizindua kozi hiyo Nape amesema kuwa,kitendo cha kuzinduliwa kwa programu mpya chuoni hapo ni jambo kubwa sana  kwa maslahi ya nchi na linapaswa  kuigwa  na vyuo vingine ili kuweza kupata wataalamu wengi zaidi waliobobea katika fani hiyo.
Nape amesema kuwa,kuwepo kwa programu hiyo katika chuo hicho kutasaidia kupata wataalamu bora na wa kipekee  waliobobea na kuondokana na changamoto  ya kuwa na wanataaluma  katika fani  hiyo ambao hawajabobea  katika maswala ya habari.
Aidha Waziri Nape aliuomba uongozi wa  chuo hicho kufikiria namna ya kuanzisha kozi fupifupi ambazo zitawawezesha wale ambao walishapitia kozi zingine kuweza kujifunza zaidi huku wakiahidi  kutoa ushirikiano kwa chuo hicho   ili kuhakikisha jambo hilo linafika mbali  zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha ,Prof Eliamani  Sedoyeka amesema kuwa,chuo hicho katika mwaka wa masomo 2023/2024 wanatarajia kuanzisha kozi mpya tano ambapo kati ya hizo kozi za shahada ni nne na moja ya shahada ya Uzamili.
Amesema kuwa ,kuanzishwa kwa kozi hizo kunafanya  IAA kuwa na jumla ya kozi 71 ambapo kati ya hizo kozi 16 ni ngazi ya cheti,kozi 17 za stashahada ,kozi 24 za shahada na kwa upande wa shahada ya Uzamili ni kozi 14.
Naye Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo cha Uhasibu Arusha,Dk Mwamini  Tulli  amesema kuwa,ubunifu uliofanywa na chuo hicho ni jambo kubwa na linapaswa kuigwa na vyuo vingine kwani kuanzishwa kwa kozi hiyo ni kuona umuhimu wa kutoa fursa kwa vijana wa kitanzania kusoma shahada hiyo muhimu katika tasnia ya habari na mawasiliano.
Ameongeza kuwa, uzinduzi wa shahada hiyo unadhihirisha jinsi chuo hicho kinavyowekeza  katika kutoa elimu bora  na kukidhi mahitaji ya wakati ,ambapo ametoa wito kwa wazazi pamoja na walezi  kukitumia  vizuri chuo hicho kuhakikisha wanapeleka  watoto wao kujifunza zaidi.
Mwisho.